Taasisi za fedha nchini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kama Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) zimejipanga kukabiliana na wimbi la wizi wa kutumia mtandao ambao umekuwa tishio hasa katika sekta hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wamiliki wa Benki nchini (TBA), Pascal Kamuzora, aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano mkuu wa chama hicho.
kwa habari zaidi....
Kamuzora aliwaeleza waandishi wa habari kuwa utekelezaji wa kukabiliana na tatizo hilo unatarajia kuanza mwakani.
Aidha, alisema katika mkutano huo, walijadili kuhusu upatikanaji wa fedha ambazo zitatumika kukabiliana na tatizo hilo pamoja na mambo mengine.
Alisema tayari walishafanya semina ambazo zilishirikisha Jeshi la Polisi, (Takukuru) na wadau wengine ili kuona namna gani watakavyofanya kazi kwa pamoja katika kukabiliana na tatizo hilo.
Aidha, alisema walikubaliana lazima wajidhatiti kwa kuanzisha taasisi maalum itakayofuatilia wizi huo wa kimtandao.
"Tumeanza kwa kuratibu wa bodi alafu baadaye tutaendelea na mambo mengine, tunaamini ushirikianao huu utatusaidia kukabiliana na tatizo hili," alisema.
Alisema benki zitaangalia namna zitakavyowawezesha wateja wake kuingia kwenye soko la pamoja la Afrika Mashariki (EAC).
Alisema katika hilo benki hazitakubali kubaki nyuma hivyo zitakuwa zikishiriki kwenye kila jambo ili watanzania nao waweze kunufaika na soko hilo kupitia sekta hiyo ya fedha.
Pia alisema katika mkutano huo walimchagua Mkurugenzi Mtendaji Benki ya Taifa ya Biashara nchini (NBC), Laurence Mafuru kuwa Mwenyekiti mpya baada ya aliyekuwa akishika nafasi hiyo kumaliza muda wake.
Mwenyekiti aliyemaliza muda wake baada ya kushika nafasi hiyo kwa muda wa miaka mitatu, Ben Christiaanse alizishauri benki nchini kutumia teknolojia za kisasa kuzuia tatizo hilo la wizi wa mtandao.
"Kila benki inasera yake na imejiwekea majukumu na malengo hivyo lazima ijiwekee mfumo utakaowasaidia kukabiliana na tatizo hilo, "alisema.
Akizungumzia kuhusu benki zilizopo nchini Uholanzi ambako ndipo anakotoka, alisema zimekuwa na mfumo wa kuzuia wizi kama huo.
Mwenyekiti mpya wa TBA, Mafuru alisema wataendelea kuhakikisha kila mteja wao ananufaika na huduma za kibenki wanazozitoa kwao.