Kipa chaguo la kwanza wa timu ya taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’, Juma Kaseja, ametajwa na makocha wengi kuwa ni kipa wa kiwango cha juu na kwamba kama tuzo za kipa bora zingezingatia kiwango cha hatua ya makundi pekee ya michuano ya Kombe la Chalenji, yeye angestahili zawadi ya kwanza.
Katika mechi tatu za hatua ya makundi, Kaseja alifungwa goli moja pekee, sawa na kipa wa Rwanda, Jean Luc Ndayishimiye, anayeidakia pia klabu ya APR nchini kwao.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, makocha wa timu za taifa za Rwanda, Mghana Sellas Tetteh, kocha wa Malawi, Kinnah Phiri na mwenzao wa Zambia, Muitalia Dario Boneti, walisema kuwa kwa mtazamo wao, Kaseja ni kipa aliyeonyesha kiwango kizuri sana katika hatua ya makundi ya michuano ya Chalenji.
Tetteh alisema kuwa uzuri wa Kaseja golini ni pamoja na uwezo wake katika kuwapanga mabeki wa timu yake katika muda wote wa mechi na vile vile amekuwa akiwakumbusha mabeki kila anapoona kuwa wanajipanga vibaya katika kuwakabili wapinzani wao.
"Ukiondoa kipa wa timu yangu (Rwanda), kipa wa Tanzania (Kaseja) yuko katika nafasi ya juu, anaonekana ni mzoefu na anaisaidia mno timu yake," alisema Tetteh, kocha aliyewahi kuipa timu ya taifa ya vijana wa umri wa chini ya miaka 20 ya Ghana ubingwa wa dunia.
Kocha wa Zambia, Boneti, ambaye timu yake iliondolewa katika michuano ya Chalenji na Ethiopia baada ya kukubali kipigo cha 2-1 juzi, alisema kuwa Tanzania ina wachezaji wengi wazuri, lakini anaamini kuwa kipa wao (Kaseja) ndiye mhimili wa safu yao ya ulinzi.
"Ni kipa mzuri, kama ningekuwa nafundisha klabu, ningependa kufanya naye kazi," aliongeza.
Phiri pia alimtaja Kaseja kuwa ni mmoja wa wachezaji watakaoisaidia Tanzania katika harakati zake za kufika mbali katika michuano mbalimbali ya kimataifa.
Msimu uliopita wa ligi kuu, Kaseja alichaguliwa kuwa kipa bora lakini msimu huu, kipa huyo mzoefu anakabiliana na ushindani mkali kutoka kwa kipa wa Yanga, Mghana Yaw Berko, aliyeruhusu magoli mawili pekee kutinga langoni kwake hadi sasa katika mzunguko wa kwanza wa ligi hiyo ya juu kuliko zote nchini.