Operesheni ya kusaka wahalifu iliyoanzishwa na Mbunge wa Vunjo, Augustine Mrema, jimboni mwake imeibua uasi mkubwa baada ya kundi la watu wanaodhaniwa kuwa ni wahalifu sugu kijijini humo kuchoma moto nyumba ya Mwenyekiti wa kijiji cha Kiraracha Kata ya Marangu Magharibi Wilaya ya Moshi, Andrew Anselim Lekule (50).
Katika mkasa huo mbaya kuwahi kutokea kijijini hapo, moto huo umemuua mke wa Mwenyekiti huyo, Catherine Andrew Lekule (45) na mtoto wake, Flora Lekule (6) pamoja na mifugo yote iliyokuwa ndani ya nyumba hiyo.
Habari zilizopatikana katika maeneo hayo zinasema kuwa tukio hilo ni kama kulipiza kisasi.
kwa habari zaidi....
Tukio hilo ambalo lilitokea Disemba 12 saa nne usiku linadaiwa kuwa lilifanywa na kundi linalosadikiwa kuwa ni wahalifu ambao walikuwa wakijinadi kabla ya tukio hilo kuwa watamkomesha Mwenyekiti huyo kutokana na hatua yake ya kuungana na Mrema kutokomeza uhalifu katika kijiji hicho. Akisimulia tukio hilo, Mbunge wa jimbo Mrema alisema baadhi ya watuhumiwa wamekwisha kukamatwa na kusema kuwa operesheni ya kuwasaka wengine inaendelea.
Aidha, alisema kabla ya kutokea kwa tukio hilo, yeye (Mrema) akiwa na mwenyekiti huyo wa kijiji walikuwa katika mikutano na waumini wa madhehebu ya Kikristo katika parokia na sharika zinazozunguka kijiji hicho katika kuhamasisha suala la polisi jamii (Sungusungu).
Alisema siku hiyo walifanikiwa kutembelea vijiji mbalimbali ikiwemo Komalyangoe, Komela, Ndueni, Kyala na kijiji cha Kiraracha ambacho wahalifu hao waliamua kumvamia mwenyekiti huyo na kumchomea nyumba yake wakati mkewe na mtoto wakiwa ndani wamelala.
“Siku ya Jumapili nilikuwa nazunguka na Andrew na saa tatu usiku tuliagana, nilipofika nyumbani tu nikaambiwa mwenyekiti wangu kachomewa nyumba na nilipoenda nilikuta amejeruhiwa huku nyumba imeteketea yote na mkewe na mtoto wakiwa wameshapoteza maisha …. Inahuzunisha, lakini pia tumewakamata watu watano ambao walihusika na tukio hilo,” alisema Mrema.
Aliongeza kuwa Jeshi la Polisi limekuwa msaada mkubwa kwao kwani usiku huo Kamanda wa Polisi na Mkuu wa Polisi Wilaya walifika na kushirikiana nao katika msako ambapo alisema walifanikiwa kuwatia mbaroni watu hao.
Hata hivyo, Mbunge huyo aliiomba serikali kuangalia namna ya kumsaidia mwenyekiti huyo kutokana na nyumba yake kuteketea kwa moto pamoja na vitu vyote vilivyokuwemo ndani.
Alisema nyumba hiyo iliteketea pamoja na nyumba ya kaka yake Michael Lekule iliyokuwa jirani.
Akithibitisha kukamatwa kwa watuhumiwa hao Kamanda wa Polisi Mkoa, Lucas Ng’hoboko, aliwataja kuwa ni pamoja na Joseph Augustine Mrema (42) Severine Ambrose (45) wote wakazi wa Kiraracha.
Wengine ni Philipo Aloyce (24), Cosmas Augustine (40) na Augustine Shayo (24) wakazi wa Makokeni. Tangu achaguliwe kuwa Mbunge, Mrema amekuwa akiendesha operesheni ya kusaka vibaka, wauza gongo na wahalifu wengine, na hivi karubuni akishirikiana na polisi walimkamata mwenyekiti mmoja wa kijiji kwa tuhuma za kushiriki katika biashara ya gongo.