Mgogoro unaohusisha umeme nchini, umezidi kupamba moto baada ya Mbunge wa Kigoma Kusini (NCCR-Mageuzi), David Kafulila, kutangaza kusudio lake la kutaka kuwasilisha hoja binafsi bungeni kuhoji sababu zinazoifanya serikali isiwajibike kwa kuliingizia taifa hasara ya mabilioni ya fedha kwenye sekta hiyo ya nishati.
kwa habari zaidi....
Amesema vilevile atawasilisha hoja hiyo, kulitaka Bunge liazimie kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja.
Amesema hoja hiyo ataiwasilisha katika Mkutano wa Bunge wa Februari, mwakani na kusisitiza kuwa iwapo atakataliwa kufanya hivyo, atashtaki suala hilo kwa wananchi.
Kafulila, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa NCCR-Mageuzi, alitangaza kusudio hilo alipozungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana kuhusu hatua anazoona zinapaswa kuchukuliwa ili kuupatia ufumbuzi mgogoro huo.
“Kwa kuwa taifa linaingia hasara kubwa ya mabilioni ya fedha kutokana na udhaifu wa serikali kusimamia mikataba na mpango mzima wa nishati, nakusudia kuepeleka hoja binafsi bungeni katika Bunge la Februari ya kwanini serikali isiwajibike kwa kuliingiza taifa hasara kwenye sekta ya umeme,” alisema Kafulila.
Aliongeza: “Pamoja na mambo mengine na kama Bunge litaona inafaa, nitalitaka Bunge liazimie kupiga kura ya kutokuwa na imani na Waziri wa Nishati na Madini kwa kushindwa kusimamia utekelezaji wa sera ya nishati na mpango wa kabambe wa usambazaji umeme na hivyo kusimamia migawo mitatu ndani ya miaka miwili ya uongozi wake.”
Alisema msingi mkubwa wa tatizo la umeme nchini, ni serikali kufumbia macho miradi ya umeme ya uhakika, ambayo ingetoa majibu ya kudumu ya tatizo hilo, badala yake imebaki kusimamia sekta ya nishati hiyo kwa kudunduliza ikitumia mitambo ya kukodi kwa miaka sasa.
Kafulila alisema mitambo hiyo ni ya tangu kampuni ya IPTL mwaka 1994 hadi ya kampuni za Aggreko, Songas, Richmond na Dowans, ambayo alisema imekuwa ikinyonya uchumi wa taifa.
Pia alisema asilimia 86 ya mapato ya Shirika la Umeme Nchini (Tanesco), yamekuwa yakitumika kulipia umeme unaozalishwa na mitambo ya kukodi inayozalisha takriban asilimia 45 tu ya umeme wote.
Mbunge huyo alisema hivi sasa mitambo ya kukodi inayotumika ni ya Songas na IPTL peke yake baada ya Aggreko kumaliza mkataba na Dowans kufutwa mkataba wake.
Alisema Tanesco wanailipa kampuni ya Songas takriban Sh. milioni 266 kila siku kwa kununua megawati 186 za umeme, wakati mitambo ya IPTL ikiwa imewashwa, wanainalipa kampuni hiyo Sh. milioni 300 kila siku.
“Itakumbukwa kuwa Tanesco walikuwa wanapaswa kuilipa kampuni ya Richmond/Dowans Sh. milioni 152 kila siku kwa kununua megawati 100 za umeme,” alisema Kafulila.
Alisema tangu mwaka 2006, serikali imeshindwa japo kupunguza tatizo la mgawo wa umeme na kwamba, viongozi wakuu wa serikali, hasa Waziri wa Nishati na Madini, mara kadhaa wamekuwa wakipotosha Watanzania kuwa serikali inashughulikia na kwamba, mgawo wa nishati hiyo utakuwa historia.
Hata hivyo, Kafulila alisema siku hadi siku sekta ya umeme imevuka upeo wa viongozi hao kiasi cha kauli zao kupoteza imani kwa Watanzania.
Alisema wakati hivi sasa Watanzania wakiwa wanazungumza mgawo wa umeme, pembeni wanakabiliwa na deni la zaidi ya Sh. bilioni 185, ambazo kwa uamuzi wa Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa (ICC), wanapaswa kuilipa Dowans, ambayo mpaka sasa serikali imekosa ujasiri kusema mmiliki wake ni nani, lakini imekiri kushindwa kesi mahakama ya kimataifa.
“Kwamba serikali isiyomjua wala kutambua uhalali wa mmiliki wa kampuni ya Dowans iko tayari kukiri kwa Watanzania kuwa kampuni hiyo isiyojulikana mmiliki wake imeshinda kesi?” alihoji.
Aliongeza: “Ni dhahiri kuwa Mahakama ya Kimataifa yenye kuheshimika duniani kote haiwezi kukaa na kushiriki katika shauri ambalo kampuni inayoshitaki haijulikani. Suala la umiliki wa kampuni ya Dowans limekuwa likichezewa tu kwa maslahi ya makambi ya kisiasa ndani ya chama tawala.”
Alisema mkataba huo ulikuwa ni wa miezi 24 na wenye thamani ya Sh. bilioni 172, lakini kwa ukosefu wa uongozi na siasa duni ndani ya mfumo wa utawala, serikali inalipia Sh. bilioni 185 tena bila kupata umeme.
“Kinachosumbua hapa ni kwamba inawezekanaje serikali kushindwa kesi na kampuni ambayo tulielezwa mkataba wake ni batili,” alisema.

Mbali na kuwasilisha hoja binafsi bungeni, pia ameitaka serikali kuona mgawo wa umeme kwamba unaathiri maendeleo kuliko hata mtikisiko wa uchumi, hivyo ifanye maamuzi magumu kwa kutenga fedha za kutosha kutekeleza mradi mkubwa wa umeme wa uhakika.
Baadhi ya miradi hiyo, alisema ni kama ule wa Stigler’s Gorge wa megawati 2000, Mnazi Bay (megawati 300) na kufufua Kiwira (megawati 200).
“Miradi yote hii inaweza kuendeshwa na sekta binafsi iwapo tutaweka mazingira mazuri ya uwekezaji,” alisema na kuitaka Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kuachana na kujenga majengo, badala yake ijielekeze kwenye uwekezaji wa uzalishaji umeme ili kutatua kabisa tatizo la umeme nchini.
Pia, alisema kwa kuwa serikali ndiyo iliyoielekeza Tanesco kuingia mkataba na Richmond na baadaye kuuhamisha kwa Dowans na Bunge ndilo lililotoa azimio la kuvunjwa kwa mkataba, shirika hilo lisibebeshwe chembe ya lawama katika suala hilo.
Alisema mzigo huo ni wa serikali unaotokana na ukosefu makini, woga na kutowajibika kiuongozi kwa viongozi wa serikali.
Hivyo, alisema serikali haipaswi kujitenga na gharama zinazotokana na madhaifu ya Tanesco katika hatua zote kwani ndio msingi wa matatizo yote ya Tanesco na hivyo inawajibika kubeba deni lote.
Vilevile, alisema kwa kuwa serikali itapaswa kulipa deni hilo kutoka fedha za walipakodi wa Tanzania na fedha hizo zitaondolewa katika bajeti ya elimu, afya nakadhalika, ni lazima serikali itoe maelezo ya kina ya sakata zima mpaka kufika lilipofika.
Alisema haiwezekani serikali itumie kodi ya wananchi kulipa deni la mabilioni ya fedha kwa kampuni, ambayo imeshindwa kuthibitisha uhalali wake na hata kutaja mmiliki wake.
Waziri Ngeleja alipotafutwa kutoa maelezo kuhusiana na madai ya Kafulila, alimuelekeza mwandishi ampigie baada ya nusu saa, lakini baada ya hapo simu yake ilikuwa haipatikani.