Baada ya klabu za Simba na Yanga kubeba mzigo mkubwa wa gharama za kutumia viwanja vya mikoani kwa mechi zao za nyumbani za ligi kuu ya Tanzania Bara, hatimaye vigogo hao wameamua kupeleka kilio kwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo Dk. Emmanuel Nchimbi ili awasaidie kupata idhini ya kuutumia Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Katika maombi yao watakayofikisha wakati wa mazungumzo na Waziri Nchimbi, Simba na Yanga zinataka ziruhusiwe kuutumia uwanja wa Taifa kuanzia mzunguko wa pili wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara utakaoanza Januari 15.
Akizungumza kwa niaba ya klabu hizo, Afisa Habari wa Yanga, Louis Sendeu, alisema kuwa viongozi wa klabu hizo walikutana juzi jijini Dar es Salaam na kujadili mambo mbalimbali, lakini hilo la kuwasilisha maombi ya uwanja wa Taifa kwa Waziri likionekana kupewa nafasi ya juu.
Sendeu alisema kuwa klabu hizo zitaiwakilisha nchi mwakani katika mashindano ya kimataifa na hivyo kuendelea kutumia viwanja vya nje ya Dar es Salaam kutaendelea kuwagharimu fedha nyingi.
Aliongeza kuwa kiufundi, endapo klabu hizo zitaendelea kutumia viwanja vya mikoani na kurejea Dar es Salaam wakati wa mechi za kimataifa, wataathirika kwani nao watakuwa wageni wa uwanja kama watakavyokuwa wapinzani wao.
Aliongeza kuwa watakapokutana na Waziri, pia wanatarajai kupata taarifa sahihi kuhusiana na hatua ya matengenezo iliyofikiwa kwenye uwanja wa Uhuru ambao walikuwa wameshauzoea kwa mechi zao za ligi.
"Vile vile klabu zinaendelea kutumia fedha nyingi kuandaa timu na tunachokipata katika mechi za mikoani ni kidogo, tutawaomba watupe uwanja huo wa Taifa na ikishindikana, basi waturuhusu tuutumie uwanja wa Uhuru," alisema Sendeu.
Akizungumzia kusudio la Simba na Yanga la kutaka kuwasilisha kwake ombi la uwanja, Waziri Nchimbi akiongea kwa njia ya simu kuwa klabu hizo zinatakiwa kufuata taratibu na hakuna kisichowezekana, alimradi wawe na hoja za msingi.
Baada ya kufungwa kwa uwanja wa Uhuru kwa ajili ya matengenezo wakati wa mzunguko wa kwanza wa ligi kuu, Yanga ilikuwa ikitumia Uwanja wa Jamhuri Morogoro na Simba ilicheza mechi zake za nyumbani kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza ambapo licha ya kubeba gharama kubwa za maandalizi na kuziweka timu zao huko, bado klabu hizo zilikuwa zikiambulia mapato ‘kiduchu’ ya milangoni.
Katika mechi mojawapo, Simba iliwahi kuambulia mgao wa Sh. 700,000, kiasi kinachodaiwa kuwa ni kidogo na hakitoshi hata kuitunza timu yao kwa siku moja inapokuwa jijini Mwanza.
Katika hatua nyingine, Afisa Habari wa Simba, Clifford Ndimbo, alisema kuwa viongozi wa Simba na Yanga wamekubaliana kusahau kwa muda uhasama wao wakati wa mechi za kimataifa na kushirikiana ili wapate matokeo mazuri kwa manufaa ya taifa.