Watu sita wamekufa kwa kuteketea kwa moto na wengine 11 kujeruhiwa baada ya gari walilokuwa wakisafiria kutoka Mbeya kwenda wilayani Makete kupinduka na hatimaye kuwaka moto.
Tukio hilo lilitokea saa 5.00 asubuhi, lilihusisha gari aina ya Land Rover, ambalo hata hivyo namba zake za usajili hazijajulikana kutokana na kuteketea kwa moto.
Abiria walionusurika katika ajali hiyo, ambao walijeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya, walisema ajali hiyo ilitokea katika eneo la Kimondo kata ya Ulenje Wilaya ya Mbeya Vijijini.
Gari hilo lilikuwa limebeba abiria na mafuta ya petroli juu ya ‘Keria’ na ndani.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi, alisema atatoa taarifa rasmi za tukio hilo baada ya kupelekewa na askari, ambao wapo kwenye eneo la tukio.
Hata hivyo, baadhi ya askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani waliozungumza kwa simu katika eneo la tukio, walisema waliokufa ni watu sita, kati yao watoto wadogo wawili na wakubwa wanne.
Mmoja wa majeruhi alisema moto huo ulikolezwa na mafuta ya petroli, ambayo yalikuwa yamepakizwa juu ya ‘keria’ baada ya kupasuka kutokana na ajali hiyo.
Katika tukio lingine, watu wawili wamefariki dunia na wengine 15 kujeruhiwa, baada ya lori kuligonga lori la mafuta.
Ajali hiyo ilitokea eneo la Kirinjiko Wilaya ya Same, mkoani Kilimanjaro wakati watu hao wakitokea mkoani Tanga kwenye mazishi.

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Lucas Ng’hoboko, alisema tukio hilo lilitokea Desemba 19, mwaka huu saa 4.00 usiku iliyolihusisha gari namba STJ 9431 aina ya Isuzu lori, mali ya Shule ya Sekondari ya Ufundi Moshi.

Alisema gari hilo lililokuwa likiendeshwa na Romwadi Kasingi (46) lilipofika katika eneo la Kirinjiko, liligongana na lori la mafuta lenye namba za usajili T. 800AGR Scania liliokuwa likiendeshwa na Valerian Mmari (40).

Waliofariki katika ajali hiyo waliokuwa kwenye lori la shule hiyo, walitajwa kuwa ni Jamila Omary (27) ambaye alifariki akiwa njiani akipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Same na Safina Msuya (56), aliyefariki wakati akiendelea na matibabu hospitalini hapo.

Ng’hoboko alisema majeruhi 13, wamelazwa hospiotalini hapo na kwamba, majeruhi wawili wamelazwa katika Hospitali ya Rufaa ya KCMC na hali zao zinaendelea vizuri.