WATU watatu akiwemo mwanamke kutoka katika wilaya za Kilombero, Ulanga na Kilosa mkoani Morogoro, wamejinyonga hadi kufa kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo za kifamilia siku ya sikukuu ya Krismasi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Adolfina Chialo, alisema hayo jana mjini hapa, na kueleza kuwa tukio la kwanza lilitokea Desemba 26, mwaka huu wilayani Kilosa ambako kijana wa Kihehe, Emmanuel Edward (25), alikutwa amejinyonga kwa kutumia kamba ya mkonge eneo la nje ya makazi yake.
Hata hivyo, Kamanda huyo alisema Edward hakuacha ujumbe wowote juu ya uamuzi wake wa
kujinyonga na Polisi inaendelea kufanya uchunguzi kuhusu tukio hilo.

Katika tukio jingine la kujinyonga, mwanamke Yoramali Muhakwi (55) ambaye pia ni Mhehe, mkazi wa Kijiji cha Chita, Kata ya Mngeta wilayani Kilombero, alikutwa amejinyonga nyumbani kwake bila ya kuacha ujumbe wowote na hivyo Polisi inaendelea na uchunguzi zaidi kuhusu tukio hilo.

Mbali na watu hao wawili, Kamanda huyo alisema mtu mwingine mwanamume ambaye hakutambuliwa jina lake wala umri, mkazi wa Ihowanja wilayani Ulanga, alikutwa
amejinyonga juu ya mti.

Hata hivyo, Kamanda huyo alisema chanzo cha mtu huyo kujinyonga hakijafahamika kwa vile hakuacha ujumbe wowote juu ya uamuzi wake na Polisi inaendelea kufanya uchunguzi juu ya vifo vya watu hao.