Hali ya usalama imeimarishwa nchini Afrika Kusini huku kukiwa na wasiwasi mkubwa kuhusiana na afya ya aliyekwua Rais wa nchi hiyo Nelson Mandela.
Polisi walishika doria wakati msongamano wa magari ukiongezeka kwenye jengo lililoko mjini Johannesburg na huku waandishi wa habari wakiendelea kumiminika nje.Hata hivyo chama kinachotawala cha ANC kimetoa wito kwa raia wa Afrika Kusini kuwa watulivu.
Watoto wa shule wamepeleka ujumbe nje ya hospitali ya Milpark wakimtakia kila la heri.
Kiongozi huyo mashuhuri anayejulikana na raia wengi wa Afrika Kusini kwa jina jingine la Madiba, ameonekana akidhoofika kiafya anapojitokeza kwa umma.
Hata hivyo kiongozi huyo tangu ajiuzulu kutoka siasa mwaka wa 2004, hajakuwa akitokea hadharani sana.
Mara ya mwisho kuonekana hadharani ilikuwa kwenye hafla ya kufunga mashindano ya Kombe la Dunia, mwezi Julai mwaka jana.
Marafiki wake wa karibu wanaonya kuwa afya ya Mandela imekuwa ikizorota kwa kasi katika kipindi cha miezi michache iliyopita.
Hali yake ya afya imekuwa kivutio kikubwa kwa wanahabari na sasa polisi wanachunguza magari yanayoingia kwenye hospitali hiyo kuhakikisha kwamba hakuna waandishi.
Mkewe, Graca Machel pamoja na watu wengine wa familia yake walionekana wakiingia kwenye hospitali hiyo Jumatano usiku.
Msemaji wa chama cha ANC amesisitiza kuwa Mandela, mwenye umri wa miaka 92 si kijana tena na hivyo atapatwa na maradhi yanayoambatana na umri wake lakini akaomba watu kutokuwa na hofu yoyote.