Kundi la watu wasiojulikana limevamia nyumba ya Mbunge wa Jimbo la Kisarawe, mkoani Pwani, Selemani Jafo, iliyopo eneo la Bomani mjini hapa, na kuiba vitu kadhaa vikiwemo vya ndani.
Mbunge alisema jana kuwa tukio hilo lilitokea majira ya saa 8:00 usiku wa kuamkia jana, wakati yeye akiwa jijini Da es Salaam, ambako alikuwa akihudhuria semina ya wabunge.
Alisema waliobaki nyumbani hapo akiwemo mkewe walishtukia makufuli na vitasa vikiwa vimevunjwa na baadhi ya vitu kama redio, televisheni kuibwa kuibwa.
Wezi hao pia walikula baadhi ya vyakula vilivyopikwa kwa ajili ya maandalizi ya siku inayofuata.
Alisema alishangazwa na wizi huo kutokea eneo ambalo viongozi wengi wa serikali wanaishi na kufafanua kuwa tayari amekwisha kutoa taarifa polisi.
Mbali na kuiba nyumbani kwa Mbunge huyo, kundi hilo pia linadaiwa kuwa usiku wa kuamkia jana lilivunja maduka 17 yaliyopo kwenye mitaa ya mji wa Kisarawe, na kuiba bidhaa mbalimbali.
Mmoja wa wamiliki wa maduka hayo, Neema Abuu Semhando, alisema alipofika asubuhi kufungua duka lake alishangaa kuona limevunjwa na baadhi ya vitu kuibwa, yakiwemo maspika makubwa ya redio.
Kundi la vijana wapigadebe katika kituo cha mabasi Kisarawe baada ya kupata taarifa hizo, lilingia mitaani na kumkamata anayedaiwa kuwa kinara wa kundi wezi.
Mmoja wa wapigadebe hao, Toshi Kiberenge, alisema mtu huyo alikamatwa katika nyumba aliyoipanga iliyopo Pugu Kigogo Fresh akiwa na baadhi ya vitu ambavyo vinatiliwa shaka kuwa ndivyo vilivyoibwa kwa Mbunge.
Polisi wilaya ya Kisarawe wamethibitisha kuwa mtuhumiwa huyo amekabidhiwa katika kituo cha polisi kituo cha wilaya kwa uchunguzi zaidi.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Pwani, Abson Mwakyoma, hakupatikana kuthibitisha tukio hilo kutokana na simu yake ya kiganjani kuita bila kupokewa.
Mkuu wa wilaya hilo, Hanifa Karamagi, alipotafutwa, alisema alikuwa katika shughuli ya kuhamasisha utumiaji wa vyandarua.
MAJAMBAZI YATEKA BASI, YAJERUHI ABIRIA

Wakati huo huo, watu 10 wanaosadikiwa kuwa ni majambazi, wameteka basi la kampuni ya Falcon Executive Ltd lililokuwa limetoka Bukoba kwenda Dar es Salaam na kujeruhi, kupora abiria, mali mbalimbali na fedha taslimu vikiwa na thamani ya mamilioni ya fedha.
Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Singida, Rajabu Bakari Muhuwila, alisema abiria hao walikatwa katwa kwa mapanga na kupigwa kwa mawe sehemu mbalimbali za miili yao.
Kwa mujibu wa Muhuwila, takribani robo tatu ya abiria wa basi hilo walikuwa ni raia wa Uganda. Basi hilo lilianzia Kampala, Uganda kupitia Bukoba.
Hata hivyo, Bakari alisema kuwa tukio hilo lilitokea juzi kati ya saa 5:00 na saa 6:00 usiku kwenye mlima wa Sekenke, uliopo Kata ya Shelui, wilayani Iramba.
Alisema abiria wanane akiwemo dereva wa basi hilo namba T.386 AUD aina ya Scania, Omari Mzee, wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Singida.
Hali ya dereva Omari Mzee ndiyo mbaya na hadi sasa bado hajajitambua. Ofisa Upelelezi wa Mkoa pamoja na baadhi ya askari wetu wamekwenda kwenye eneo la tukio na wakirudi nitawapatieni taarifa sahihi yenye kuonyesha thamani ya mali na fedha zilizoporwa na majambazi hayo,” alisema.
Mmoja wa abiria hao, Lutaya Richard, ambaye ni raia wa Uganda aliyekuwa anasafiri kwenda Zimbabwe, alisema walipokaribia kumaliza kupanda mlima Sekenke, walikuta lori aina ya semi trela na mbele kulikuwa na mawe makubwa katikati ya barabara.
Aliongeza kuwa pembeni yake dereva wa lori hilo alikuwa amelazwa chali huku jiwe kubwa likiwa limewekwa juu ya tumbo lake.
Alisema baada ya basi lao hilo kusimama ndipo ghafla watu hao walijitokeza na kuanza kupiga mawe madirisha ya basi na kuharibu madirisha yote ya upande wa kulia.
Hata hivyo Richard alisema baada ya kuharibu madirisha hayo ndipo walipotoa amri kwamba abiria wote washuke chini huku wakinyanyua mikono yao juu.
Baada ya kushuka chini, amri nyingine ilitolewa kwamba tutoe simu zetu zote na fedha tulizonazo tuwakabidhi wao...amri hiyo tuliitekeleza kwa kuhofia usalama wa maisha yetu,” alisema.
Aalisema kuwa aliporwa fedha za Afrika Kusini Rand 4,000 (sawa na Sh. 832,000) na simu moja ya kiganjani.
Kwa ufupi ni kwamba abiria wameporwa kati ya Shilingi 200,000 hadi milioni tano taslimu na wengine wameporwa Dola za Marekeni za mamilioni ya fedha,” alisema huku machozi yakimtiririka na kuongeza:
Kwa sisi abiria kutoka Uganda kwa kweli hakuna aliyebakiwa na akiba yoyote, tumeporwa kila kitu hata nyaraka zetu za kusafiria.”
Na kibaya zaidi ni kwamba tulikuwa hatuelewi amri zilizokuwa zikitolewa na majambazi hayo kwa vile wengi wetu hatukuwa tukikifahamu Kiswahili, tunajua Kiingereza tu,” alisema.
Mfanyabiashara Mtanzania, Joyce Daniel, aliyekuwa akitokea mjini Kampala kununua mali ambayo alikuwa akiipeleka jijini Dar es Salaam, alisema yeye alifanikiwa kuwatoroka watu na kwenda kuficha fedha zake na simu yake ya mkononi porini.
Binafsi nawasikitikia mno hawa ndugu zetu kutoka Uganda hawakuwa na ujanja wameporwa kila kitu pamoja na hati zao za kusafiria ... kwa sasa hawana hata senti ya kununulia kikombe cha chai ya rangi,” alisema Joyce.
POLISI WAUA WATUHUMIWA WA UJAMBAZI
Katika tukio lingine, watu wawili wanaosadikiwa kuwa majambazi wameuawa katika mapambano na jeshi la polisi katika wilaya ya Kibondo, mkoani Kigoma.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kigoma, George Mayunga, alisema kuwa watu hao walikuwa ni miongoni mwa watu wanane na kwamba tukio hilo lililotokea usiku katika msitu ulioko kati ya vijiji vya Bunyambo na Kumhama karibu na mpaka na Burundi.
Alisema baada ya polisi kupata taarifa kutoka kwa wananchi, waliweka mtego na kuwapata majambazi hao wakiwa njiani ambapo baada ya kuwasimamisha waligoma na kuanza kurushiana risasi na kwamba tukio hilo lilifanikisha pia kukamatwa kwa bunduki mbili aina ya SMG na risasi 270.
Alisema majambazi hao kwa mujibu wa taarifa waliyozopata kutoka kwa baadhi ya wananchi, walikuwa wakipanga kuteka mabasi na magari yanayopita katika barabara kuu ya Kasulu-Kibondo hadi Nyakanazi.

Kwa mujibu wa Mayunga, maiti za watu hao ambao hazijatambulika, lakini wanasadikiwa kuwa raia wa Burundi na kwamba zimehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kibondo.