HIVI karibuni halmashauri mbalimbali hapa nchini zilikamilisha mchakato wa kupata wenyeviti wa halmashauri za wilaya, miji na mameya wa manispaa na majiji ili waanze kazi za kuleta maendeleo kwa wananchi.
Makala haya yaliyoandikwa na ROSE MUYENJWA wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) yanaelezea kwa undani umuhimu wa kazi zinazofanywa na halmashauri na Serikali za Mitaa hapa nchini.

ILI kuleta maendeleo katika wilaya, tarafa, kata, kijiji na hata mtaa ni jukumu la kila
Mtanzania kutambua wajibu wake na kuutekeleza ipaswavyo, akishirikiana na viongozi husika
kama madiwani.

Pamoja na uwapo wa madiwani na viongozi wengine katika Serikali za Mitaa, ni wajibu wa
serikali kuchunguza mfumo mzuri unaoweza kuleta manufaa na maendeleo katika jamii ili
ulete tija kwa kila mwanajamii kujituma na kutekeleza wajibu wake.

Profesa Suleiman Ngware na George Chale waliandika kuhusu mfumo wa Serikali za Mitaa katika kitabu cha; ‘Diwani na Maendeleo’, wakieleza mambo mbalimbali juu ya mfumo huu, yakiwamo majukumu na wajibu wa diwani na uwezo wake katika kusimamia na kubuni shughuli za maendeleo katika kata zao.