JESHI la Polisi mkoani hapa, limekamata bunduki ya kivita katika mji mdogo wa Kaliua iliyokuwa ikitumiwa na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Tabora, Liberatus Barlow, amesema, silaha hiyo ya kivita ilikamatwa Kaliua, wilayani Urambo.

Amesema, Polisi wa doria, walikuta vijana tisa, wakijiandaa kufanya uhalifu Kaliua.
Polisi walipofika eneo la uwanja wa michezo wa Kaliua, walikuta vijana hao tisa waliokuwa wamevalia makoti marefu, wamepumzika wakijiandaa kufanya uvamizi na uporaji.

Hata hivyo, baada ya kuona askari, vijana hao walikimbia na hivyo kuacha bunduki aina ya SMG na risasi 30 kwenye magazini yake, ambapo askari Polisi waliwakimbiza na kupiga risasi angani lakini hakuna aliyekamatwa.

Amesema, hata hivyo usiku huo askari hawakuiona ila waliporudi kukagua eneo la tukio asubuhi wakaikuta imetelekezwa kwenye majani.

Amesema, bunduki hiyo namba CT 18731998 licha ya kuonekana ni chakavu, lakini imekuwa ikitunzwa na inafanya vizuri katika utendaji wake, kwa kuwa ipo salama kiufundi.

Amesema, eneo la Kaliua, limekuwa likisumbua kwa matukio ya ujambazi kutokana na kuwa na misitu mingi na katika baadhi ya maeneo hakuna mtandao wa simu, kitu ambacho kimewafanya majambazi kujichimbia zaidi katika maeneo kama hayo.

Hata hivyo, amesema Polisi imekuwa ikitegemea sana dhana ya Polisi Jamii ambayo imesaidia kupunguza uhalifu na kwamba Jeshi hilo litaendelea kutumia mbinu mbali mbali hadi litakapofanikiwa kukomesha ujambazi.