WAKATI bado anakabiliwa na kesi ya kufanya maandamano bila kibali mjini Arusha, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, ameingia matatani kwa mara nyingine, safari hii Mahakama ya Wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro imeamuru akamatwe.
Mbowe ambaye pia ni Mbunge wa Hai, anatakiwa akamatwe kwa madai ya kushindwa kufika mahakamani kujibu mashitaka yanayomkabili.


Hati hiyo ilitolewa Machi 18, baada ya Mbunge huyo kutohudhuria mahakamani hapo, bila taarifa wala mdhamini wake.

Hakimu Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Denis Mpelembwa, aliagiza kutolewa kwa hati hiyo, baada ya Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Inspekta Kassim Mgwambi kutoa maelezo ya kutohudhuria kwa mtuhumiwa mahakamani hapo, bila hivyo kukiuka masharti ya dhamana.

Mwendesha mashitaka alisema, pamoja na kutoa hati ya kumkamata mshitakiwa huyo, pia alitoa hati ya kumkamata mdhamini wake na kuandikiwa barua ya kuitwa mahakamani kutokana na kushindwa kufuata masharti ya kumdhamini mtuhumiwa huyo.

Awali ilidaiwa kuwa, Mbowe anakabiliwa na mashitaka ya kufanya vurugu na kumjeruhi Msimamizi wa Uchaguzi, siku ya uchaguzi mkuu katika kituo cha Lambo Oktoba 31 mwaka jana.

Inadaiwa mshitakiwa huyo alimshambulia msimamizi huyo, Nasri Othmani na kumsababishia maumivu makali mwilini.

Mbowe ameshitakiwa kutokana na kuvunja kifungu cha sheria ya makosa ya jinai kifungu cha 240 sura ya 16 ya sheria za Tanzania kutokana na kufanya shambulio hilo katika kijiji hicho saa 11 jioni.

Pamoja na kutolewa hati ya kumkamata mshitakiwa huyo kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa Mei 8.

Kwa sasa, Mbowe na viongozi wengine wakuu wa Chadema, wanakabiliwa na mashitaka ya kuongoza maandamano mjini Arusha yaliyolenga kupinga uchaguzi wa Meya wa Manispaa hiyo.