Wakuu wa vyombo vya habari wapatao 100 wakiwemo wahariri, wachapishaji na waandishi wa habari maarufu kutoka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), watakutana kwa siku mbili mjini Nairobi, Kenya, kujadili nafasi ya vyombo vya habari katika kuimarisha ushirikiano wa jumuiya hiyo.
Mkutano huo utakaoanza leo, umeandaliwa na EAC kwa kushirikiana na Baraza la Biashara la Afrika Mashariki (EABC).

Pamoja na mambo mengine utajadili fursa zinazopatikana kwa vyombo vya habari katika mwendendo mzima wa ushirikiano huo na nafasi ya vyombo hivyo katika kujenga uelewa wa wananchi wa kawaida juu ya michakato mbalimbali ya kuimarisha jumuiya hiyo.
Mada kuu ya mkutano huo ni mchango wa vyombo vya habari katika kuimarisha ushirikiano wa kikanda na maendeleo, lakini pia wajumbe wanatarajiwa kujadili kwa kina rasimu ya sera ya mawasiliano yenye lengo la kuimarisha taasisi za kanda na kuongeza usambazaji wa habari za EAC ili kuwafikia wananchi.
Rasimu hiyo ya sera ya mawasiliano itakapokamilika itawasilishwa mbele ya Baraza la Mawaziri wa EAC, ambalo ni chombo cha juu cha maamuzi ili iweze kupitishwa rasmi. Nchi wananchama wa EAC ni pamoja na Kenya, Uganda,Tanzania,Rwanda na Burundi.
Miongoni mwa watu wengine mashuhuri watakaoshiriki mkutano huo ni pamoja na Katibu Mkuu wa EAC anayemaliza muda wake, Balozi Juma Mwapachu, Spika wa Bunge la Afrika Mashariki Abdirahin Abdi na Mwenyekiti Mtendaji wa Makampuni ya IPP, Reginald Mengi, ambapo Waziri Mkuu wa Kenya Raila Odinga anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika tukio la utoaji wa tuzo.