MWANAFUNZI wa darasa la tano katika shule ya msingi wilayani Temeke mkoani Dar es Salaamm (jina limehifadhiwa), amejinyonga.
Mwanafunzi huyo alijinyonga baada ya baba yake mzazi kumuadhibu kwa sababu ya utoro wa shule.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile amesema, maiti ya mtoto huyo mwenye umri wa miaka 15, ilionekana juzi saa 12 asubuhi Kiwalani, wilayani Ilala katika nyumba mbovu iliyopo katika majengo ya Mamlaka ya Hali ya Hewa. “Alikutwa amejinyonga katika banda bovu katika majengo ya hali ya hewa kwa kutumia kamba ya katani ambayo aliitundika kwenye dari,” alisema Kamanda Shilogile.

Kamanda Shilogile alisema , kwa mujibu wa maelezo ya baba mzazi wa mtoto huyo, Tajiri Mbegu (53), ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa Kiwalani Migombani, mwanafunzi huyo alitoroka nyumbani kwake tangu Machi 11 mwaka huu baada ya kumuadhibu kwa tabia yake ya kukataa kwenda shule.

“Baada ya hapo mzazi huyo alidai kwamba alimweleza mtoto wake kwamba kesho yake wataongozana kwenda shule wakaonane na walimu wake na kuanzia hapo mtoto huyo hakuonekana tena hadi alipokutwa akiwa amejinyonga,” alisema Kamanda Shilogile.

Maiti ya mwanafunzi huyo amehifadhiwa katika Hospitali ya Amana na polisi wanaendelea na upelelezi.