BUNGE wa zamani wa Musoma Mjini, Vedastus Manyinyi, ameahidi kuwalipia nauli ya kwenda na kurudi Loliondo wakazi 130 wa mjini Musoma ili wakapate tiba.
Amesema hayo wakati akihutubia mamia ya wakazi wa hapa kwenye viwanja vya shule ya msingi Nyakato kuwashukuru kwa kuichagua kwa kura nyingi CCM na kumwezesha Rais Jakaya Kikwete kuibuka mshindi.
“Nimekuja kuwashukuru kwa dhati kwa uamuzi wenu wa kuendelea kumchagua Rais Kikwete na CCM kuongoza nchi kwa awamu ya pili, lakini niwashukuru wote walionichagua kwa kura walizonipa ingawa hazikutosha,” alisema.

Manyinyi alisema, asiyekubali kushindwa si mshindani na yeye alikubali matokeo na kusisitiza kuwa hizo ndizo siasa za kiungwana zinazohitajika sasa.

“Nimeamua kuwasafirisha wananchi wa Musoma 130 ili wakatibiwe, orodha ya majina ya watu watakaokwenda nitaipata kutoka kwa Mbunge wenu, Vincent Nyerere (Chadema) na nitawaandikia barua Meya wa Manispaa na Mbunge kuwaarifu hilo ili watoe kibali cha ninyi kwenda kutibiwa,” alisema na kuongeza:

“Watu wengine wakishindwa, huamua kukataa matokeo, lakini mimi niliyekuwa Mbunge wa Musoma Mjini na mgombea kwa tiketi ya CCM, nilikubali matokeo na mmeona hakukuwa na fujo na katika kipindi changu nilifanya kazi bila kuchoka.

Alisema, licha ya kwamba hakuchaguliwa kuwa Mbunge ana mengi ya kujivunia, ikiwa ni pamoja na alivyokuwa akiendesha mikutano yake ya kijimbo baada ya kutoka bungeni.

“Mbunge ni yule anayeitisha vikao na wananchi wake kabla na mara baada ya mkutano wa Bunge ili achukue mawazo yao na kuyapeleka bungeni, hiyo kazi niliifanya kikamilifu,” alijisifu.

Wananchi hao wa Musoma watakwenda Loliondo mkoani Arusha kupata tiba ya magonjwa mbalimbali inayotolewa kiimani na Mchungaji mstaafu Ambilikile Mwasapile, ambaye anatoza Sh500 kwa kikombe cha dawa hiyo.