Siku mbili tu baada ya wananchi kuchachamaa kufuatia tangazo la serikali la kusitisha huduma ya tiba inayotolewa na Mchungaji Mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambikile Mwasapile, sasa imeibuka na kusema huduma hiyo haijasitishwa.

Kauli ya awali ilitolewa Jumatano wiki hii na Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Haji Mponda, kwamba alikuwa amemwagiza Mganga Mkuu mkoa wa Arusha kusimamia kazi ya kisitisha utoaji wa huduma hizo nyumbani kwa Mchungaji huyo kijijini kwake Samunge, Loliondo, wilayani Ngorongoro, Mkoa wa Arusha, hadi kamati ya uchunguzi aliyounda kwenda kuchunguza mazingira ya utoaji tiba hiyo itakapokamlikisha kazi na kutoa ripoti.
Jana katika hatua mpya, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi, alisema serikali haijasitisha huduma ya tiba inayotolewa na Mchungaji Mwasapile.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana Lukuvi alisema zoezi la utoaji wa huduma hiyo itaendelea kama kawaida hadi idadi kubwa ya watu walioko huko imalizike.
“Serikali haijazuia na haina mpango wa kuzuia tiba inayotolewa na Mwasapile kwa kuwa inaendana na mambo ya imani ambayo haina mamlaka ya kuyaingilia, isipokuwa sisi tunachoomba wananchi watuelewe sasa hivi ni kwamba idadi ya watu walioko kule mpaka sasa ni 6,000, tunataka hao wamalizike kwanza halafu ndio tutatoa taarifa ili wengine waende,” alisema. Lukuvi alisema hiyo ni tahadhari ambayo inachukuliwa mapema katika kukaribia kipindi cha masika ili kuepusha kuzuka kwa magonjwa ya mlipuko kutokana na mrundikano mkubwa wa watu eneo hilo.
Alisema hivi sasa ulinzi umeimarishwa katika barabara zinazoingia eneo hilo ili kuhakikisha hakuna magari yanayopita wala watu wanaoingia mpaka watakapohakikisha watu waliopo huko wamepatiwa tiba na kuondoka ndipo wawaruhusu wengine.
Aliongeza kuwa hivi sasa wanafanya mawasiliano na Machungaji Mwasapile ili kujua idadi kamili ya watu anaoweza kuwahudumia kwa siku, ambao ndio watakaokuwa wanakwenda kupatiwa matibabu kila siku.
Waziri Lukuvi alisema taarifa kuhusiana na ratiba za tiba hiyo itakuwa inatolewa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Isdore Shirima, kupitia vyombo vya habari. “Tumeomba Mwasapile atwambie idadi kamili ya watu anaoweza kuwahudumia kwa siku, ili tuhakikishe idadi hiyo ndiyo inaenda na siyo watu wote kurundikana huko kwa mara moja, kwa sababu hatutaki tiba hiyo izue balaa badala ya kutibiwa wakaambukizana magonjwa,” alisema Lukuvi.
Akizungumzia kuhusiana na tiba hiyo, Lukuvi alisema wamepata shuhuda kutoka kwa watu mabalimbali ambao wamethibitisha kuanza kwake siku nyingi na kwamba iliwaponya.
“Sisi hatujasema tunaikubali wala tunaikata tiba hii kwa sababu hata hivyo, tumepata shuhuda kutoka kwa watu mbalimbali ambao wanasema wameponywa na tiba hiyo siku nyingi, na mmoja wao ni Askofu wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Kati, Thomas Laizer, na endapo ingekuwa inadhuru wasingekuwa wanaishi mpaka sasa, na hatuwezi kusema ina sumu wala haina, sababu hayo ni mambo ya kitaalamu na huyu Mwasapile naye ameoteshwa,” alisema.

TIMU YAUNDWA KUSIMAMIA ULINZI
Aidha, Lukuvi alisema hivi sasa imeundwa timu maalum ya kusimamia suala la ulinzi na usalama ambayo inasimamiwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha na tayari ilianza kazi jana.
Alisema moja ya vitu vitakavyosimamiwa na timu hiyo ni pamoja na kuhakikisha kuwa hakuna mbinu zozote za ujanjaujanja zitakazotumiwa na watu wanaoingia sehemu hiyo, madereva wanaowatoroka abiria wao au wale wanaopandisha nauli za kwenda sehemu ya matibabu.
Aliongeza kuwa serikali imeagiza kupelekwa jopo la wataalamu wa afya pamoja na gari (ambulance) kwa ajili ya kusaidia kutoa huduma za wagonjwa mahututi kuwapekeka katika vituo vya afya vilivyopo karibu na eneo hilo.
Alisema watauomba uongozi wa KKKT ambao upo eneo hilo kutoa huduma, kushirikiana na jopo la watu wa afya ili kusaidiana katika utoaji huduma hiyo.
Lukuvi pia amemshukuru Mwasapile kwa ushirikiano ambao ameutoa kwa jopo la wataalamu ambao walikwenda kufanya uchunguzi wa tiba ambao walirejea jana jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuanza kazi ya kuchunguza dawa hiyo.
Alisema tayari amewaonyesha wataalamu hao mti unaotumika kutengenezea dawa hiyo.
Alisema uchunguzi umeshaanza ili kubaini jina la dawa hiyo, usalama wake pamoja na kuangalia masuala ya matumizi sahihi ya dozi.
Hata hivyo, aliwaomba wananchi ambao wamekwisha kunywa dawa hiyo kwenda katika maabara za afya za serikali, kuhakiki afya zao kama watakuwa wamepona kwa kufuata siku walizoambiwa na Mwasapile.

MADAKTARI WAIZUNGUMZIA DAWA
Baadhi ya madaktari bingwa wa magonjwa sugu yakiwemo yanayodaiwa kupata tiba kwa mchungaji Mwasapile wamewashauri watu wanaosumbuliwa na maradhi hayo kuepuka ushabiki kuhusiana na matumizi ya dawa za asili ili malengo na matarajio yao yaweze kutimia.
Madaktari hao akiwemo Dk. Josiah Mlay wa Hospitali ya Mkoa wa Arusha Mount Meru na Dk. Julius Msuya wa Hospitali ya St. Thomas pamoja na kuthibitisha kuwa dawa za asili zina nafasi yake katika tiba ya magonjwa mbali mbali, wamesema zinaweza kuwaumiza wagonjwa badala ya kuwasaidia kama ushabiki utatawala katika utoaji na utumiaji wake.
Wamesema kwa ujumla imani inaweza kumfanya mgonjwa apate nafuu ama apone kabisa na pia kumfanya azidiwe hivyo ni vyema wenye mamlaka ya kutoa maamuzi wakalizingatia hilo.
Kuhusu madai ya kuwepo kwa baadhi ya wagonjwa wanaotoroshwa mahospitalini na kupelekwa kwa kupata tiba hiyo, Dk. Mlay alisema katika Hospitali ya Mount Meru hilo halijajitokeza. “Tumekuwa tukisikia maneno mengi, lakini hapa kwetu hakuna kilichobadilika, idadi ya wagonjwa wanaoingia na kutoka ni ile ile na pia wanaoomba ruhusa ya aidha kuwahamisha wagonjwa wao ama kuwarudisha nyumbani ni ile ile,” alisema. Hata hivyo, Dk. Mlay amewashauri wanaofikia uamuzi wa kubadili mwelekeo wa tiba kutoka dawa za hospitali kwenda kwenye dawa za mitishamba kuwa makini na kuepuka ushabiki wa maneno ya mitaani.
Dk. Julius Msuya alisema matumizi ya dawa za mizizi yanatambulika kote duniani, lakini bado taratibu na tahadhari juu ya utaratibu wake zinahitajika.
“Suala la msingi ni kujua zinatibu nini na kwa kiwango gani na suala la mtu kuchagua aina ya tiba ni la mtu mwenyewe, cha msingi cha kuangalia ni jinsi zinavyoweza kumsaidia,” alisema Dk. Msuya.

WATU WAENDELEA KURUNDIKANA
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Raimond Mushi, amesema bado kuna mrundikano mkubwa wa wagonjwa kwa Mchungaji Mwasapile na zipo taarifa kuwa wengine wengi wanaendelea kwenda na kwamba jitihada za kuepusha madhara yanayoepukika hasa yanayoweza kutokana na msongamano zinaendelea.
Pia, Mushi ameungana na watalaamu wa afya kulaani hatua ya baadhi ya watu ya kuwatorosha wagonjwa waliozidiwa kutoka mahospitalini ama majumbani na kuwasafirisha katika mazingira magumu na ya hatari, amewataka wanaofanya hivyo kuacha mara moja kwani watakuwa wanawaumiza wagonjwa wao badala ya kuwasadia.