Kiongozi wa Libya Kanali Muammar Gaddafi alisema watu wake watapambana iwapo nchi za magharibi au Umoja wa Mataifa zitazuia ndege zao kupita kwenye anga ya nchi hiyo, kama waasi wengi nchini humo walivyopendekeza.

Katika mahojiano na televisheni ya Uturuki, alisema kuzuia ndege kupita angani humo kutadhihirisha wazi nia yao ya kutaka kunyang'anya mafuta.
Wakati huo huo, majeshi yanayomwuunga mkono Gaddafi yalishambulia vitongoji vya Zawiya na kujaribu kudhibiti eneo la wazi.
Marekani imesema uamuzi wowote wa kuzuia ndege kuruka kwenye anga ya Libya umebaki mikononi mwa Umoja wa Mataifa.
Zaidi ya watu 1,000 wanaaminiwa kufariki dunia tangu waasi walipoanza ghasia takriban wiki tatu zilizopita ili kumwondoa Kanali Gaddafi aliyekaa madarakani kwa miaka 41.
Umoja wa mataifa unakadiria kuwa takriban watu 212,000, wengi wakiwa wafanyakazi wahamiaji-wameondoka nchini humo.