Balozi wa Marekani nchini, Alfonso Lenhardt, ametoa changamoto kwa wanaume wa Tanzania kuwaunga mkono na kuwatia moyo wanawake katika shughuli zao mbalimbali wanazozifanya ili waweze kutoa mchango wao kwa jamii kwa ukamilifu.
Lenhardt aliyasema hayo jijini Dar es Salaam kwa waandishi wa habari alipokuwa akiitambulisha semina ya uongozi kwa wanawake wa Tanzania iliyoandaliwa na kufadhiliwa na ubalozi huo.

Alisema kwamba zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania wote nchini ni wananwake na wengi wao wana akili, uwezo, ujasiri wa kufanya mambo ya msingi ambayo kama wataungwa mkono watachangia vya kutosha katika ustawi wa nchi hii.
“Wanawake wa Tanzania wanaonyesha njia,wakiwasaidia wanawake wenzao namna ya kujikwamua katika maisha. Tanzania ina wanawake wengi wa kupigiwa mfano ambao wamejipambanua toka zamani katika nyanja zote za kijamii. La msingi ni kutowakatisha tamaa bali kuwaunga mkono,” alisema.
Alisema kuwa anafahamu kuwepo kwa mazingira mbalimbali yanayosababisha ugumu kwa wanaume wa kutambua na kuukubali uwezo wa wanawake, lakini alisema hali ya sasa imebadilika na inaruhusu haki ya wanawake kufikia upeo wa ufanisi wao.
Leihardt alisema kuwa katika sekta zote za kibiashara, kwenye mashirika, asasi mbalimbali, serikalini ambako kuna wanawake, kazi zao zimefanyika katika kiwango cha juu na hivyo kuchangia katika mapato ya familia, jamii na nchi kwa ujumla.
Awali, mshiriki wa semina hiyo, Joy Kemibaro, alisema kwamba amepata manufaa mengi yatakayorahisisha utendaji wake wa kazi.
Alisema semina hiyo imemuwezesha kukutana na wanawake wenzake ambao alikuwa hafahamiani nao kubadilishana nao mawazo na imempa somo la namna ya kuendesha nguvu zake.
Naye Irene Kiwia, mshiriki mwingine alisema maono yake ni kuwa mwanamke anayejitegemea kiuchumi na kijamii na hivyo mafunzo hayo yamempa njia za kufikia malengo yake.
Semina hiyo iliendeshwa na wakufunzi wawili toka Marekani, Mary Davis Holt na Jill Flynn ambao wapo nchini tangu Machi 20, mwaka huu.
Wanatarajiwa kuendesha semina nyingine katika Jiji la Arusha.