Wanafunzi watatu wa Shule ya Sekondari Malengwelengwe, Kata ya Mngazi Wilaya ya Morogoro wamekufa papo hapo na wengine 17 kujeruhiwa kwa kupigwa na radi wakati wakiwa shuleni
Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Said Mwambungu, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo Machi 24, mwaka huu majira ya saa 11:00 jioni.
Mwambungu alisema kuwa wanafunzi hao waliokufa walikuwa wanasoma kidato cha kwanza shuleni hapo.
Aliwataja kuwa ni Abdalah Kibwe, Kunambi Adolph na mmoja aliyefahamika kwa jina moja Ambias.

Akizungumzia kuhusu majeruhi hao, alisema wawili wamelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Morogoro kutokana na hali zao kuwa mbaya.
Alisema wengine walitibiwa katika zahanati ya Mngazi na Kituo cha afya Dutumi kisha kuruhusiwa kutoka baada ya hali zao kuwa nzuri.
Alisema tukio hilo lilitokea shuleni hapo wakati mvua kubwa zkinyesha huku zikiwa zimeambatana na radi na upepo mkali
" Wakati tukio hilo likitokeza wanafunzi wengine walikuwa madarasani na viwanja vya michezo wakijiandaa na mashindano ya Umoja wa Michezo kwa Shule za Sekondari (Umiseta)," alisema Mwambungu.
Katika tukio jingine; Salma Rashid Madenge, mkazi wa kijiji cha Lukurunge kata ya Mvuha wilayani humo amekufa kwa kuliwa na mamba.
Mkuu huyo wa Wilaya, alisema tukio hilo lilitokea majira ya usiku Salma akiwa na mumewe shambani wakilinda mazao yao yasiharibiwe na wanyama.
Alisema ghafla alitokea mamba huyo na kumkamata kisha kumvutia hadi ndani ya bwawa lililopo jirani na shamba hilo.
Alisema mume wake huyo alifanya jitihada za kukabiliana na mamba hiyo lakini alimshinda baada ya kumzidi nguvu.
Baada ya jitihada za kumuokoa mkewe kukwama, alipiga yowe kuomba msaada na kusababisha wananchi kujitokeza na kuanza kumsaka mamba huyo," alisema na kuongeza kuwa hawakufanikiwa kutokana na bwawa hilo kuwa na mamba na kiboko kuwazidi nguvu.
Kutokana na tukio hilo, Mwambungu alimwagiza Afisa Maliasili wa Wilaya ya Morogoro kwenda katika eneo hilo ili kuutafuta mwili wa mwanamke huyo na kuukabidhi kwa ndugu kwa ajili ya mazishi.