Makamu wa Rais Dk. Mohammed Gharib Bilal akisoma hotuba yake katika Baraza la Idd el-Hajj baada ya swala ya Idd iliyofanyika kitaifa kwenye Msikiti wa Al Farouq Kinondoni, Dar es Salaam. (Picha na Muhidin Sufiani).

BARAZA Kuu la Waislamu wa Tanzania (BAKWATA) limezipongeza Serikali ya Tanzania na ya Mapinduzi Zanzibar kwa kupinga ushoga na ndoa za jinsi moja na kusema, ni heri kufa njaa kuliko kushibishwa kwa kudhalilishwa.

Pia Bakwata imeahidi kuendelea kuunga mkono Serikali kwa misimamo yake ya kukataa kusaidiwa kwa masharti yasiyojali wala kuheshimu utu na thamani ya Mtanzania, kwa sababu ina lengo zuri la kuutetea utaifa.

Akizungumza katika Baraza la Idd el Hajj katika Msikiti wa Masjid Al Farouq, Kinondoni jana, Shehe wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum alisema, heri kuwa tayari kufa kwa njaa kutokana na umasikini, kuliko kupewa misaada ya maendeleo kwa masharti ya kudhalilishwa utu.

Kwa mujibu wa Shehe Salum, Serikali zote mbili zimeonesha kutokuwa na woga katika kulinda na kutetea heshima ya raia wake, jambo linalostahili pongezi za dhati na kuungwa mkono.

“Kwa kueleza misimamo yao dhidi ya kauli ya hivi karibuni ya Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron kuhusu mpango wa nchi yake kuzinyima misaada nchi masikini, ikiwemo Tanzania, endapo hazitaruhusu ushoga na ndoa za jinsi moja Waziri Membe (Bernard) na Rais wa Zanzibar (Dk. Mohamed Shein) wameonyesha thamani ya Mtanzania kwa watu wa Magharibi.

“Bakwata tunaungana nao kuukataa ushoga na ndoa za jinsia moja kwa sababu sio utamaduni wetu wala jambo sahihi kwa maadili ya Mtanzania,” alisema Shehe huyo.

Wakati huo huo, Kaimu Mufti wa Tanzania, Shehe Muhidin Mkoyogore, aliwataka Watanzania wadumishe upendo miongoni mwao, ili wasitoe mwanya kwa watu wa nje kujipenyeza kuvuruga amani nchini, kama ilivyotokea Libya na katika nchi mbalimbali zenye machafuko Afrika.

Mkoyogore alisema, kukosekana kwa upendo miongoni mwa watu wa taifa moja, hasa katika Afrika ni udhaifu unaotoa nafasi kwa mataifa ya Magharibi kujipenyeza na kubomoa amani iliyopo kwa njia za kurubuni na uchochezi wa machafuko.

“Mwalimu Julius Nyerere ametuachia urithi wa amani katika nchi yetu sasa sio vema kuuacha upotee kwa kuruhusu mataifa ya nje yatutenge na kutuingiza katika migogoro kama iliyotokea Libya…msikubali kwa sababu madhara ya vita yatabaki kwetu na sio kwa wachochezi,” alisema.

Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal aliitaka Bakwata iongeze shule nyingi zaidi, ifungue vituo vya afya na kuhamasisha vijana kujiunga na ujasiriamali, kwa kuwa inayo nafasi nzuri ya kufanya hivyo.

“Kama chombo cha dini mnawajibu wa kuisaidia Serikali kuhakikisha maadili mema kwa raia. Kuheshimiana ni chanzo cha amani katika nchi hivyo tumieni fursa mlionayo kuhamasisha amani na maadili mema miongoni mwa Watanzania, pamoja na kuwahamasisha vijana kujiunga na ujasiriamali.

“Najua mnatakiwa kuongeza nguvu kusomesha vijana wetu katika elimu zote yaani ya dini na elimu dunia hivyo jengeni shule nyingi zaidi na kufungua vituo vya afya Watanzania wafaidike,” alisema Dk. Bilal.

Naye Jasmin Shamwepu anaripoti kutoka Dodoma kwamba Waislamu mkoani Dodoma wamelaani vikali ndoa ya jinsi moja na kueleza kuwa jambo hilo halikubaliki kwa mujibu wa dini ya Kiislamu na hata katika dini nyingine.

Shehe wa Mkoa wa Dodoma, Mustafa Rajabu Shaaban aliwaambia waumini waliokusanyika kwenye msikiti wa Gaddafi mjini Dodoma kuwa ndoa za jinsi moja hazikubaliki hata kijamii na kimataifa.

Alisema jambo hilo lilisababisha watu kuangamizwa na Mwenyezi Mungu; “Mwenyezi Mungu alishusha laana na maangamizi kutokana na uchafu wa kuwaingilia wanaume kinyume na maumbile.

“Waislamu tunakemea vikali kitendo hicho (tamko la Cameron) na kwa mafundisho ya dini ya Kiislamu hatukubali upuuzi huo kwa sababu jambo hili litakapotokea, linaweza kusababisha Machafuko.

“Hawa (Waingereza) wasijione kuwa wao ni wafalme wa dunia kwa kutaka kila wanalosema likubaliwe hata kama litakuwa baya kwa kisingizio cha misaada yao,” alisema.

Kiongozi huyo wa dini alisema Waislamu wanaunga mkono Serikali kwa kuonyesha ujasiriwa kukemea madikteta wa nchi za Magharibi na kupinga vikali kauli hiyo iliyotolewa na waziri Mkuu wa Uingereza.

“Uingereza ni moja ya nchi za Magharibi ambazo bado zinafikra za kikoloni, kibeberu na kidikteta ambazo zimekuwa mstari wa mbele kutumia kisingizio cha haki za binadamu kuvamia nchi ambazo zinaendelea ikiwemo Libya kwa malengo ya kuendeleza ubabe wake na kuiba rasilimali za nchi hizo ikiwemo mafuta, madini na gesi,” alidai.