Katibu wa Wabunge wa Chadema, John Mnyika.

Waungana na NCCR kuwasha moto nje
Wabunge CCM, CUF wawashambulia

Wakati mjadala wa Muswada wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2011 ukiendelea huku mashambulizi ya wabunge wengi wa CCM na CUF yakielekezwa dhidi ya wale wa Chadema.
Jana wabunge wa Chadema na wa NCCR-Mageuzi, walikutana nje ya Bunge mjini hapa na kutangaza rasmi kuwa hawatashiriki mchakato huo na kwamba wameazimia kwenda kuwajulisha wananchi sababu za kuukataa.
Hayo yalisemwa jana na Katibu wa Wabunge wa Chadema, John Mnyika, pamoja na wabunge wa NCCR-Mageuzi, walipozungumza na waandishi wa habari mjini hapa.
Wabunge wa NCCR-Mageuzi waliofikia uamuzi huo, ni Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila na Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali.
“Ni suala zito la kitaifa na lenye kugusa maslahi ya wananchi bila kujali itikadi ya vyama vya siasa. Tumeona umuhimu wa jambo hili kupelekwa kwa mahakama ya wananchi. Hoja zetu zikaenda kwa wananchi,” alisema Mnyika.
Mnyika alisema kutokana na jitihada hizo kuhitaji pia msukumo wa kisiasa, walikubaliana kukiomba chama kuitisha kikao cha Kamati Kuu ya dharura.
“Chama kimekubali na kikao maalum cha kamati kuu cha dharura kitafanyika kesho na mahali ambapo tutawatangazia hapo baadaye baada ya kukamilisha taratibu zote,” alisema Mnyika.
Alisema kamati kuu ya chama chake kama chombo cha juu cha uongozi kitaeleza juu ya hatua, ambazo zitachukuliwa na chama kuhusu jambo hilo.
Mnyika alisema sababu ya kutokubali kushiriki katika mjadala huo mbali na kuwepo mapungufu katika vifungu vya muswada huo ni kutoshirikishwa kwa wananchi na Bunge kulazimisha kusomwa mara ya pili badala ya mara ya kwanza.

Alisema pia wameshangazwa na kauli ya Spika wa Bunge, Anne Makinda, alipoombwa mwongozo na Mbunge wa Mbozi Mashariki (CCM), Godfrey Zambi, kuhusiana na wabunge wa Chadema kutoshiriki mjadala wa muswada huo baada ya kutoka ndani ya Bunge.
Awali, kabla ya Bunge kuahirishwa jana mchana, Zambi alihoji kama Spika ana taarifa kuhusiana na tangazo la wabunge wa Chadema kutoshiriki katika mjadala.
“Tumeshangazwa na mwongozo alioutoa spika wa kusema kwamba yeye kama spika hafahamu wabunge wa Chadema na wa NCC-Mageuzi waliotoka bungeni hawatashiriki mjadala. Tumeshangazwa na taarifa hiyo kwa sababu kauli ya kukataa kushiriki mjadala endapo utasomwa kwa mara ya pili ipo ndani ya ofisi ya Bunge,” alisema na kuongeza:
“Lipo kwenye hansard (kumbukumbu rasmi za Bunge), na imetolewa kama sehemu ya hotuba ya kambi rasmi ya upinzani, ambayo kwa tafsiri ya marekebisho ya kanuni, inajumuisha wabunge wote wa upinzani. Kwa hiyo msimamo uliwekwa bayana katika hotuba iwapo serikali itaendelea na azma hii ya kufanya muswada huo ujadiliwe kwa mara ya pili, sisi hatuko tayari kushiriki ukiukwaji huu wa kanuni za Bunge, ukiukwaji wa Katiba ya Nchi na tulizitaja ibara, ibara ya nane, 18,26, 146 na 63.”
Kwa upande wake, Kafulila alisema walilazimika kuchukua hatua ya kukataa kuchangia muswada huo kwa ajili ya kuweka kumbukumbu kuwa hawakushiriki katika mchakato wa kutunga sheria hiyo.
Alisema muswada huo ulikwenda kutafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ili ueleweke kwa Watanzania na waweze kuujadili kabla ya kuingia bungeni.
“Mnaweza kuwauliza hawa watu wa Chama Cha Mapinduzi. Huu muswada uliotafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili ni lini umepelekwa kwa wananchi, kwa sababu lengo la kufanya hivyo ni wananchi waweze kuelewa. Kwa sababu kama wabunge kupitisha muswada siku zote wanapitisha miswada iliyoandikwa kwa lugha ya Kiingereza,”alisema.
Alisema hakuna namna yoyote ya kuubadilisha muswada huo wakiwa ndani ya Bunge.
“Tutakwenda kwa wananchi kuwajulisha mawazo yetu kwanza ya kukataa ule muswada na sababu za kufanya hivyo. Lakini tunachokiepuka kushiriki katika mchakato huo ni kuwa ungehalalisha uamuzi wenye hila, ambao walikuwa wanataka kuufanya kupitia Bunge la Tanzania.
“Kwa kuwa wanataka kuufanya na wameshaupanga kufanya hivyo, waufanye wao wenyewe, wajadiliane wao wenyewe, wapige kura wao wenyewe, lakini sisi mikono yetu isiwe sehemu ya hiyo dhambi. Sasa kuna mawazo kwamba miswaada mingine tunajadili, tunafikia hitimisho hata kama wao ni wengi nataka niwaambie kuwa kuna umaalumu wa kutengeneza Katiba itakayoishi zaidi ya miaka 100 hadi 200.”
Jana wabunge wa Chadema na wawili wa NCCR-Mageuzi, walitoka ndani ya ukumbi wa Bunge, muda mfupi baada ya Msemaji wa kambi ya Upinzani kuhusiana na Katiba na Sheria kusoma hotuba yao ambayo pamoja na mambo mengine ilitaka kuahirishwa kwa mjadala wa Katiba hiyo.
WABUNGE CCM, CUF WAWASHAMBULIA WABUNGE CHADEMA
Katika hatua nyingine, wabunge wa CCM) na CUF, jana walitumia muda mrefu kuchangia muswada huo kwa kuwashambulia wanaharakati na wabunge wa Chadema kwamba, wameupotosha umma kuhusu muswada huo.
Wanaharakati kupitia Jukwaa la Katiba walikuwa wanataka muswada huo usomwe mara ya kwanza bungeni kwa maelezo kuwa ni mpya kwa kuwa umefanyiwa marekebisho makubwa baada ya kuondolewa bungeni Aprili mwaka huu, kwa lengo la kuufanyia marekebisho, ikiwa ni pamoja na kuuchapisha kwa lugha ya Kiswahili.
Kwa upande wake, wabunge wa Chadema juzi walitoka nje ya ukumbi baada ya Spika Makinda, kukataa kuwaruhusu kupewa mwongozo wakati muswada huo ulipokuwa unasomwa kwa mara ya kwanza.
Kadhalika, wabunge wa NCCR-Mageuzi, Kafulila na Felix Mkosamali (Muhambwe), nao walitoka nje baadaye na kuungana na wabunge wa Chadema.
Jana Mbunge mwingine wa NCCR-Mageuzi, Moses Machali (Kasulu Mjini), naye aliungana na wenzake kususia mjadala huo baada ya kuchangia na kusema kuwa haukupaswa kusomwa kwa mara ya pili.
Mbunge wa Tabora Mjini (CCM), Aden Rage, alilishambulia Jukwaa la Katiba, akisema linataka kulinyang’anya Bunge mamlaka yake.
Alisema lilichapisha taarifa katika magazeti ambayo alisema kuwa inatia kichefuchefu.
“Ni dhahiri wanataka kutupora mamlaka tuliyopewa pamoja na kumdhalilisha Rais,” alisema Rage na kuwaita wanaharakati hao kuwa ni wahuni.
Kauli hiyo ya Rage haikumpendeza Spika Makinda, ambaye alimtaka afute kauli yake ya kuwaita wahuni.
Rage pia alimshutumu Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani, Tundu Lissu (Singida Mashariki-Chadema), kwa hotuba yake ya juzi jioni kabla ya wabunge wa chama chake kutoka nje ya ukumbi wa Bunge, akisema muswada huo unampa madaraka makubwa Rais na kumfanya kuwa mfalme na dikteta.
Alisema hotuba ya Lissu lengo lake sio kitu kingine bali kutaka kuuvunja Muungano.
Felister Bura (Viti Maalum-CCM), alisema wanaharakati wanaoupotosha muswada huo wanawachonganisha watu na kwamba wanamtukana Rais, mawaziri na Bunge.
“Hali hiyo inatia hofu. Nani anawapa kivuli na wanachokitaka ni nini?” alihoji na kuongeza kuwa wanaharakati hao wanasema kuwa wataandamana na hakuna chombo au mtu atakayewagusa.
Mbunge wa Mkanyageni (CUF), Habib Mnyaa, alisema kumekuwapo na upotoshaji mkubwa unaofanywa na vyombo vya habari, wanaharakati na vyama vya siasa na kwamba kama upotoshaji huo utaendelea, nchi itafika pabaya na kupendekeza zichukuliwe hatua kwa wakati.
Alisema CUF hawawezi kuiacha fursa ya sasa ya kuandika Katiba mpya kwa kuwa katiba ya sasa ndiyo iliyokuwa ikiwalazimisha Wazanzibari kulalamikia mambo yaliyopo katika Muungano.
Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Ummy Ally Mwalimu, alisema wanaharakati na wanasheria wamekuwa wakipotosha muswada huo kwa kuhoji madaraka ya rais bila kuhoji tume zilizoundwa huko nyuma kama ya Jaji Nyalali na Jaji Kisanga.
Mwalimu, ambaye pia ni Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, alisema wanaharakati na wanasheria wanahoji mamlaka ya Rais katika kuunda Tume ya Katiba wakati katika nchi za Kenya, Ghana, Zambia na Uganda marais ndio waliounda tume za kuandika katiba zao.
Naibu Waziri huyo alihoji ni nani, ambaye wanamwakilisha na kuongeza kuwa kuna maslahi nyuma yaliyojificha.
Mbunge wa Simanjiro (CCM), Christopher Ole Sendeka, alimshambulia Lissu, kwamba kauli yake kuwa Rais wa kwanza wa Tanzania, Mwalimu Julius Nyerere, alimomonyoa uhuru wa Zanzibar katika Katiba na kwamba wakati wa uongozi wake haki za binadamu hazikuwekwa katika katiba.
Sendeka alisema katiba ya kudumu ya mwaka 1977 inatamka kwamba katika kuamua mambo yanayohusu katiba, lazima kila upande theluthi mbili ya wabunge wake waridhie.
Pia alisema wakati wa uongozi wa Mwalimu Nyerere mwaka 1984 ndipo hati ya haki za binadamu iliingizwa katika katiba.
Mbunge wa Wawi (CUF), Hamad Rashid Mohamed, aliwalaumu wabunge wa Chadema kuhoji madaraka ya Rais na kuongeza kuwa Rais angekuwa na nia mbaya, angeweza kuunda Tume ya Katiba bila kutaka maoni ya Bunge au mtu mwingine.
Alisema tangu aingie bungeni mwaka 1977, hajawahi kuona mchakato ulioshirikisha watu wengi kama wa muswada huo.
Mbunge wa Mbozi Mashariki (CCM), Godfrey Zambi, aliomba mwongozo chini ya kifungu cha 68 (7), juu ya wabunge wa Chadema juzi kutoka nje ya ukumbi wa Bunge wakati walipoanza kuchangia muswada.
“Na taarifa zipo kwamba kwenye mjadala huu bado hawataendelea kushiriki, lakini hivi punde Mheshimiwa Spika umetangaza kwamba Katibu wa Wabunge wa Chadema anaomba uwatangazie wabunge wa Chadema kwamba wataenda kufanya mkutano wao mara baada ya kipindi cha maswali na majibu,” alisema na kuongeza:
“Sasa mimi nikawa najiuliza hivi vyama vya siasa vitakuwa vinaruhusiwa kwenda kufanya mikutano wakati mijadala inaendelea nikajiuliza hivi Chama Cha Mapinduzi wakiomba idhini hiyo wataruhusiwa wakafanye mkutano wa chama chao wakati Bunge linaendelea, naomba mwongozo wako Mheshimiwa Spika.”
Akijibu mwongozo huo, Makinda aliusifia na kufafanua kuwa walikubaliana kuwa mikutano yote ya kishughuli ifanyike baada ya saa 7:00 mchana.
“Ni kwa woga huo huo kwamba ikifanyika wakati huo huo hapa kunawezekana kukawa hakuna watu wale ambao wanataka kufanya mikutano katikati ya kipindi cha maswali na saa 7.00 mchana, lakini kwa kutegemea na umuhimu wa hicho kitu labda kinatakiwa,” na kuongeza.”
“Katibu wa Chadema hajaomba, lakini hata ninavyosema wali walkout (walitoka nje) mimi niliona kama wanawalk out kama watu wengine wowote wale sijaambiwa rasmi kama wana walkout kwa sababu gani, kwa hiyo na mimi nilishangaa, lakini nikafikiria labda…kwa hiyo mikutano yoyote ile isipokuwa kwa idhini ya Spika inafanyika baada ya saa 7:00.”
Baada ya kutoa mwongozo huo na Katibu wa Bunge kusoma shughuli inayofuata, wabunge hao wote wa Chadema na wawili wa NCCR Mageuzi, walitoka ndani ya ukumbi wa Bunge.
Akichangia mjadala huo, Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Angela Kairuki, aliwaponda wabunge waliotoka ndani kuwa wamediriki kumbeza hayati Mwalimu Nyerere, Rais Jakaya Kikwete, Muungano na Bunge.
Alihoji watu wanaopinga muswada huo wana imani na nani kama si Rais na kuwataka waache kuwapotosha wananchi.
“Hizi ni kauli za watu waliosoma nusu nusu,” alisema Kairuki, ambaye ni Makamu Mweyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Sheria, Katiba na Utawala.
Mbunge wa Kigamboni (CCM), Dk. Faustine Ndungulile, aliwataka wabunge wenzake kutojadili kwa kuangalia itikadi, Utanzania Bara wala udini.
Alisema sasa hivi kuna madalali wa Katiba, ambao wamekuwa wakitaka kujipatia umaarufu kwa kutumia mchakato huo hali ambayo inaweza kusababisha vurugu.
“Wanaohamasisha muswada huu ukataliwe tuwapuuze …hawa wanashiriki katika kuwasilisha maoni yao halafu baada ya kuwasilisha wanasusia,” alisema.
Alisema wanaosema nchi hii kuna urais wa kifalme waende kuona nchi nyingine zenye utawala wa kifalme kuona zinavyoendeshwa.
Alisema Rais katika muswada huo, hajapewa madaraka makubwa kama wanavyosema wanaharakati, bali amebanwa kwa kupewa vigezo na sifa za kuteua kamati hiyo.
Wabunge wengine waliotoa maneno makali dhidi ya wabunge wa Chadema, ni George Simbachawene (Kibakwe-CCM), Esther Bulaya (Viti Maalum-CCM), Kapteni John Komba (Mbinga Magharibi-CCM), Margareth Mkanga (Viti Maalum-CCM), Mohamed Chomboh (Magomeni-CCM) na Yahya Kassim Issa (Chwaka-CCM).
MACHALI: UONDOLEWE
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali, jana aliungana na wabunge wenzake wa NCCR-Mageuzi na wa Chadema, akitaka uahirishwe na kwenda kutafuta maoni zaidi ya wananchi katika maeneo yote ya nchi.
Alisema malumbano yanayoendelea ndani ya Bunge na nje yanatokana na wananchi wengi wakiwamo wa jimbo lake kutopewa muda wa kutosha wa kuujadili muswada huo.
Machali alisema kinacholalamikiwa ni jinsi mchakato wa muswada ulivyoingizwa bungeni na kuongeza kuwa wananchi wanataka uwepo wigo mpana wa kukusanya maoni yao katika maeneo mengi. Alisema hawalaumu wabunge waliotoka nje kwa sababu wamekosa uvumilivu.
Alisema wananchi hawakutaka usomwe kwa mara ya pili kwa sababu hawakupanuliwa wigo kutokana na Kamati ya Bunge kutokwenda maeneo mengine zaidi ya Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar.
Machali alisema watakaopitisha muswada huo, lawama za Watanzania zitakuwa juu yao.
Baada ya kuchangia, alitoka nje akitimiza ahadi yake ya juzi kwamba alibaki bungeni ili kuipa ujumbe serikali kwamba muswada huo uondolewe.
CHANZO: NIPASHE
0 Maoni | Kuwa wa kwanza kutoa maoni