Nchini Libya mamia ya wafungwa wanaachiliwa huru kabla ya sikukuu ya Eid al-Adha, hapo kesho.
Serikali ya mpito ya Libya imekubali kuwafungua watu wanaoshukiwa walipigana upande wa Gaddafi.

Lakini wakuu wamekiri kuwa wale wanaoshukiwa kuwa ni askari mamluki wa kigeni bado wamebakizwa kizuizini ili wafikishwe mahakamani.

Mamia ya wafungwa mjini Misrata, Tripoli na miji mengine wamekuwa wakiachiliwa katika juma hili, ili kuadhimisha sikukuu ya mwanzo tangu Libya kutangazwa kuwa imeshakombolewa mwisho wa mwezi Septemba.

Jamaa wa wafungwa walikusanyika nje ya gereza ya Misrata, huku wakilia kwa furaha, na kuwapa mkono walinzi wa jela waliokuwa wamewafunga.

Wengi wao walitekwa katika mapambano ya mwisho ya kukomboa eneo karibu na mji wa Sirte kutoka wafuasi wa Muammar Gaddafi.


Walishutumiwa kuwa walipigana au kuwapa hifadhi wanajeshi wa Gaddafi.

Wakuu wa gereza la Misrata waliiambia BBC, kwamba askari wa kukodiwa hawakufunguliwa...hao ni Waafrika, raia kutoka nchi kama Chad, Mali na Niger.

Hakuna dalili kuwa wataachiliwa huru karibuni; jambo ambalo linatia wasiwasi mashirika ya kimataifa ya kupigania haki za kibinaadamu.