Tanzania haitafikia matarajio ya kujenga misingi ya demokrasia ya vyama vingi iwpo polisi watazidi kudumisha utendaji wa mfumo wa serikali za chama kimoja.
Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti Baraza la Ushauriano la Vyama vya Siasa nchini, Juma Ali Khatibu, kufuatia kukamatwa kwa baadhi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), katika mgogoro wa kisiasa mkoani Arusha.
Alisema mgogoro ni wa muda mrefu na kinachojitokeza ni utendaji wa polisi kusahau misingi ya maadili ya taluma hiyo ya kulinda usalama wa raia na mali zao.
“Kwa utendaji huu wa chombo cha dola, msingi wa demokrasia hauwezi kupatikana Tanzania hadi hapo Jeshi la Polisi litakapokubali kubadilisha mfumo wa utendaji wake wa kazi,” alisema Juma ambaye pia ni Katibu Mkuu wa Tanzania Democratic Alliance (Tadea).
Aidha alisema kwamba kwa mujibu wa sheria namba 5 ya mwaka 1992, vyama vya siasa vina haki ya kufanya mandamano lakini polisi wamekuwa kikwazo nakuwanyima haki wananchi yakufahamu kinachoendelea katika nchi yao.
Makamu Mwenyekiti huyo, alisema baraza hilo limesikitishwa na kitendo cha Jeshi la Polisi kuwakamata hovyo viongozi wa vyama vya siasa na kuwadhalilisha mbele ya wanachama wao wakati ni viongozi wa kitaifa.

Alisema Baraza hilo limeamua kukutana kujadili mgogoro wa kisiasa unaondelea kujitokeza Mkoani Arusha, ili kuepusha damu kumwagika na watu kupoteza maisha.
“Baraza tayari tumewasiliana na Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa ili kuweza kujadili matatizo ya kisiasa yanayojitokeza Arusha,” alisema.
Hata hivyo, alisema utatuzi wa migogoro ya kisiasa hauhitaji nguvu na kwmaba jambo la msingi ni viongozi wa Chadema wakae pamoja na polisi kujadili chanzo na njia muafaka za kumaliza mgogoro huo.
Upande wake, Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo, alisema wakati umefika vyama vya siasa viruhusiwe kufanya mikutano na maandamano kwa vibali badala ya kutoa taarifa kwa Jeshi la polisi kabla ya kufanyika kwa mikutano hiyo.
“Pepo mbaya katukumba tusikubali mambo ya Tunisia, Misri, Libya kwa sababu waliojaribu wamepigwa kiuchumi na kimwili,” alisema Cheyo alipozungumza na kituo kimoja cha radio cha visiwani hapa, bila kufafanua kauli yake “tupozi kidogo na maadamano sio kila siku maadamano barabarani.”
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mipango na uendeshaji sera wa Chama cha wakulima Tanzania (AFP), Rashidi Yussuf Mshenga, alisema matatizo yanayotokea Arusha hayaonyeshi mwelekeo mzuri kwa Tanzania katika kujenga misingi ya haki za binadamu na Utawala bora.
Aidha, alisema Jeshi la polisi lazima litumie busara ili kufanikisha wajibu wake wa kulinda usalama wa raia na mali zao kwa kutoa haki kwa vyama vyote vya siasa.
Mkurugenzi huyo alisema kwamba vyama vya siasa nchini kazi yake kubwa ni kutetea misingi ya demokrasia na utawala bora kwa maslahi ya taifa na wananchi wake
CHANZO: NIPASHE