Shirika la Viwango Tanzania (TBS), limeamuru kuteketezwa shehena ya mabati yasiyo na viwango yanayosambazwa na Kampuni ya Kamaka CO. Ltd iliyopo Tabata relini Barabara ya Mandela, jijini Dar es Salaam.
Shehena hiyo ya mabati ilibainika jana katika msako wa kushtukiza uliofanywa na TBS, ambapo ilibainika kuwa sehemu ya bidhaa hiyo tayari imeishauzwa katika mikoa mbalimbali.
Akizungumza katika eneo la tukio, Ofisa Masoko wa TBS, Daud Mbaga, alisema baada ya kumhoji mmiliki wa kampuni hiyo, Idrisa Coptecin, alikiri kusambaza bidhaa ambazo hazina nembo ya ubora kutoka TBS.
“Mabati haya hayana nembo ya ubora, nembo ya mtengezaji, hayana anuani wala hayaonyeshi yana geji ngapi na tumemuaru mmiliki huyo kutoendelea kuyasambaza na badala yake ayateketeze,” alisema.
Naye Ofisa Viwango wa TBS, Joseph Ismail, alisema mabati hayo yalikamatwa na baada ya kupimwa yalibainika kuwa hayana viwango vya ubora na kwamba huenda yaliingizwa nchini kwa njia za panya.
Ismaili alisema sheria inawapa uwezo wa kuzuia usambazaji wa bidhaa zinazobainika kuwa “feki” na kuamuru ziteketezwe pamoja na kuziondoa katika soko.

“Tulichukua sampuli ya mabati haya na kuyapeleka katika maabara zetu na baada ya kuyapima, tulibaini kuwa hayana ubora wa viwango ndiyo tumefika hapa na kuzuia yasiendelee kuuzwa,” alisema Ismail.
Alitaja sifa za mabati yasiyokuwa na ubora kuwa ni pamoja na kushika kutu haraka muda mfupi baada ya kuezekea nyumba pamoja na kuwa mepesi.
Aidha, Ismail alisema kampuni hiyo pia inasambaza vifaa vingine vya ujenzi ambavyo ni nondo pamoja na mabomba na kwamba TBS inaendelea kuchunguza bidhaa hizo.
Kabla ya TBS kufanya msako huo, wananchi mbalimbali walikuwa wanalalamika kwa kuuziwa mabati mabovu ambayo yalikuwa yanashika kutu muda mfup baada ya kuyaezekea nyumba zao na kuvilaumu viwanda vya ndani vinavyotengeneza bidhaa hizo.
Mmiliki wa kampuni hiyo ambaye inadaiwa kuwa ni raia wa Uturuki, Idrisa Coptecin, alikijitetea kuhusu bidhaa hizo, alikiri kuwa ni hazifikii viwango, lakini alisema kwamba na yeye aliuziwa na mfanyabishara mmoja ambaye hata hivyo, alikataa kumtaja jina lake. Alisema aliuziwa mabati 8,000 na kwamba na yeye baada ya kuyanunua alifanikiwa kuyauza kwa wateja wake kutoka maeneo mbalimbali ya nchi ambapo hadi jana alikuwa amebakiza mabati 3,000.
Wamiliki wa viwanda vya mabati nchini wamekuwa wakiwasaka wafabiashara wanaouza bidhaa feki kwa kuwa wanaharibu soko na kuwafanya wateja wao wawaone na wao ni matapeli.