Wanafunzi watatu wa kidato cha pili wa Shule ya Sekondari Ikola katika Tarafa ya Karema, wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma ya kumshambulia na kumjeruhi Mkuu wa Shule hiyo, Mwalimu Kateka Kipeta baada ya Mwalimu huyo kukataa kushinikizwa na wanafunzi wa kidato cha nne wa shule ili kuvujisha mtihani wa kidato cha nne uliofanyika hivi karibuni shuleni hapo.
Kamanda wa Polisi mkoani Rukwa, Isuto Mantage, alisema tukio hilo lilitokea wiki iliyopita majira ya saa tano asubuhi ambapo wanafunzi hao kuanzia kidato cha kwanza hadi cha tatu walifanya vurugu hizo, baada ya kuwafungia walimu wengine kwenye ofisi yao kisha kwenda kuvamia ofisi ya Mwalimu Chipeta.
Kamanda Mantage alisema kuwa wanafunzi hao walifanikiwa kuwashawishi wenzao takribani 260 na kwenda kuvamia ofisi ya mkuu wa shule na kuanza kumpiga kwa fimbo na ngumi kabla ya Mwalimu Chipeta kufanikiwa kupokonyoka na kwenda kujisalimisha kwenye ofisi ya Mtendaji wa kata hiyo.
Inadaiwa kuwa, kufuatia kipigo hicho ilibidi Mkuu wa shule akimbizwe katika zahanati ya kijiji hicho ambako alitibiwa na baadaye kuruhusiwa, baada ya kupata michubuko kwenye maeneo mbalimbali ya mwili wake.

Uchunguzi uliofanywa awali, umebaini kuwa wanafunzi hao waliamua kufanya vurugu hizo baada ya kupata malalamiko kutoka kwa wenzao wa kidato cha nne juu ya kushindikana kwa mpango wao wa kumshawishi mkuu wa shule hiyo kupokea fedha walizochanga ili amshawishi msimamizi wa mitihani ya kidato cha nne kwa lengo la kuvujisha mitihani ya mwaka 2011.
“Hawa wanafunzi wanadaiwa kuwa walichanga fedha na kumpatia mkuu wa shule yao ili ampatie huyo msimamizi, lakini mkuu wa shule hiyo alikataa kufanya kitendo hicho cha uvunjaji wa sheria hali iliyowaudhi wanafunzi hao kiasi cha kulazimika kuwaeleza wenzao wa madarasa ya chini yao walioamua kumpiga mkuu wao wa shule,” alisema Kamanda Mantage.
Hata hivyo, Kamanda huyo hakueleza sababu za kuwakamata wanafunzui watatu pekee wakati idadi kubwa ya wanafunzi wanadaiwa kwamba walihusika katika vurugu hizo za kushinikiza uongozi wa shule ukubali kuvujisha mtihani huo.