Mabaharia wa meli moja ya uvuvi ya Taiwan, wamefanikiwa kuwatimua maharamia wa Kisomali ambao walikuwa wamewateka nyara katika pwani ya Afrika Mashariki.

Mabaharia hao 28, waliwashinda nguvu maharamia hao, siku moja baada ya meli hiyo kutekwa nyara takriban kilomita 100 Kusini Mashariki mwa mji mkuu wa Somalia, Mogadishu.

Meli hiyo kwa jina Chin Yi Wen sasa inaelekea Ushelisheli huku hatma ya maharamia hao wa Kisomali ikiwa haijulikani.

Shirika la kimataifa linalosimamia safari za meli IMB, limesema kuimarika kwa hali ya ulinzi na sera bora zimepunguza idadi ya meli zinazotekwa nyara na maharamia wa Kisomali, katika kipindi cha miezi 12 iliyopita.