WATOTO 14 wamezaliwa katika mkesha wa Sikukuu ya Idd-el-Hajj katika hospitali mbili za Serikali ya Mnazi Mmoja pamoja na Mwembeladu mjini Unguja.

Kwa mujibu wa Muuguzi Mkuu wa Hospitali ya Mwembeladu, Wahida Mohammed Idrissa, watoto saba ni wavulana na saba wengine ni wasichana na wamezaliwa wakiwa katika hali ya afya njema na kuruhusiwa kurudi majumbani.

“Tumezalisha jumla ya watoto 14 katika Hospitali ya Mnazi Mmoja wakiwa na siha nzuri na tumewaruhusu akinamama kurudi nyumbani baada ya kuridhika na mazingira yao,” alisema Idrissa.

Alisema kwa mujibu wa sheria za afya, kinamama hutakiwa kukaa hospitali katika muda wa saa 24 baada ya kujifungua huku wakiangaliwa hali ya afya yao kwa karibu zaidi, lakini sasa wanakaa muda wa saa sita kutokana na kuwepo kwa msongamano mkubwa hospitalini hapo.



Alisema hali hiyo inatokana na kinamama wengi sasa kuhamasika kujifungua hospitalini zaidi kuliko majumbani.

“Hilo ndiyo tunalolitaka kwa sasa.....tumefanikiwa kuwahamasisha kinamama kujifungua katika hospitali za Serikali na kuhudumiwa na wakunga wanaotambuliwa,” alisema.

Alisema hivi sasa hata matukio ya kesi mbalimbali zinazowakumba kinamama kutokana na kujifungua kwa kiasi kikubwa yamepungua.

Mikakati hiyo inakwenda sambamba na lengo la Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuhakikisha kinamama wote wanajifungua hospitalini na kushughulikiwa kwa matibabu na madaktari wenye uwezo wa shughuli hizo ili kuepusha vifo vya watoto na kinamama.