MKAZI wa mtaa wa Maisaka Sinai mjini Babati mkoani Manyara, amenusurika kuuawa baada ya kukatwa sikio na kulazimishwa kulimeza kutokana na kipigo cha kwa wananchi, akidaiwa
kuiba mbuzi wawili na kutaka kuwauza.

Daatho Kodi (20) alipigwa na wananchi juzi saa 10 jioni, kwenye mnada wa Gendi wilayani Babati na kukatwa sikio la kushoto na kulazimishwa kulitafuna akipewa na chumvi.

Akizungumza kwa njia ya simu,mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo, Joseph Muray ambaye
alikuwa mnadani hapo, alisema kama si jitihada za Mwenyekiti wa soko hilo, Sifael Mollel, hivi
sasa Kodi angekuwa marehemu.

Muray alisema Mollel alitumia askari wa mgambo mnadani kuzuia vurugu hizo na kuwaita
polisi waliofika eneo hilo wakati Kodi ameshajeruhiwa kwa kipigo na kukatwa sikio.

Alisema watu hao walimpiga mtuhumiwa huyo aliyedaiwa kuiba mbuzi wawili, beberu na
jike, mali ya Safari Angali (24) mkazi wa mtaa wa Nakwa Barazani, Babati.



Alisema baada ya kuiba mbuzi hao aliwapeleka mnadani hapo na wakati akitafuta mnunuzi, alikamatwa na kupigwa kwa silaha za jadi.

Muray alisema alipokamatwa aliambiwa achague moja, kati ya kuuawa au kukatwa sikio na
kulitafuna na chumvi na kulimeza, akachagua sikio likatwe.

“Alipigwa kwa marungu na mapanga na kukatwa sikio na kupewa chumvi na kulitafuna na
kulimeza hadi polisi walipoitwa,” alisema shuhuda huyo.

Alidai kuwa, Kodi ni mzoefu wa kuiba mali za watu na amekuwa akikamatwa na kuachwa kutokana na kulindwa na ndugu na jamaa zake.

“Walitaka kumuua na kama si Mwenyekiti kuita polisi wangemmaliza, kwani walidai
wakimkamata huachiwa,” alisema.

Kodi anaendelea kupata matibabu kwenye hospitali ya mji wa Babati (Mrara) huku akiwa na
pingu mikononi.