VITA ya maneno na matusi makali imekolea, sura iliyopo inaonesha kuwa mastaa, Wema Isaac Sepetu na Irene Pancras Uwoya wanaweza kumtoa macho Jacqueline Wolper Masawe kufuatia tifu zito linaloendelea kati yao na mwenzao huyo, Ijumaa lina ripoti kamili.
Tayari Wema na Uwoya ‘wamemvua nguo’ Wolper wakitumia maneno makali yaliyotafsiriwa kuwa ni matusi mazito yakiwemo mnafiki, mshamba na mlugaluga aliyetimba mjini na suruali au kaptula (pedo) za drafti, drafti.

HARUFU YA DAMU YATAWALA
Wakiwa na hasira mithili ya nyumbu aliyekoswa na risasi wakiashiria harufu ya damu, juzi kupitia kipindi cha Take One cha Clouds TV kinachosimamiwa na Zamaradi Mketema, sura hizo za mauzo katika Bongo Movies walipasua jipu pwaa kuwa wamemkinai Wolper kwa tabia zake za kujivika ngozi ya kondoo ilihali ndani ni chui wa kuogopwa zizini.

WEMA
Ilishaelezwa kuwa Wema na Wolper wana bifu la muda mrefu ambalo chanzo chake ni penzi la brazameni wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul Jumaa ‘Diamond’.

Akifunguka juu ya bifu hilo, Wema alidai kuwa anamshangaa msanii huyo kwa kuendeleza umbeya na chuki binafsi zisizokuwa na maana.

NI HASIRA YA KUSALITIWA NA DIAMOND?
The Udaku Master, Ijumaa linashikilia maneno ya furaha ya Wolper juu ya madai ya Wema kumwagana na Diamond akidaiwa ‘kubanjuka’ na Miss Tanzania namba 2, 2006, Jokate Mwegelo.
 
Duru za kihabari zinadai kuwa inawezekana Wema alitumia air time kwa hasira kumchana Wolper kwa kile kinachoelezwa kuwa alimtuhumu kumuibia tunda lake kwa Diamond, lakini kumbe kulikuwa na mtu mwingine (eti Jokate).

MANENO YA SHOMBO YA WEMA KWA WOLPER:
“Wolper ni mshamba, amekuja mjini akitokea sijui Moshi au uchagani tunamuona na suruali sijui kaptula za drafti, drafti.
“Kulumbana na Wolper ni kumpa umaarufu kwani jina langu ni kubwa, hawezi kunifikia hata siku moja.
”Sidhani kama naweza kukaa meza moja na Wolper, sijui kwa kweli.”

TUJIKUMBUSHE
Hivi karibuni, Wema na Wolper walivaana kisharishari, kila mmoja akiapa kumshikisha adabu mwenzake, lakini waungwana wakawaamulia kabla mambo hayajaharibika.

DALILI ZA HATARI
Dalili za hatari na umwagaji wa damu zilishaonekana, kwani kuna watu walijigawa pande mbili, wapo waliomsapoti Wema na wengine Wolper.

SIKIA MICHANO YA UWOYA KWA WOLPER:
“Nilikuwa sitaki kumzungumzia huyo mtu, sijui Jack (Wolper), ana majina mengi sijui supastaa, any ways Jack sijui nisemeje lakini ana tabia fulani hivi.


 “Tulikuwa tunaongea vizuri, lakini siku moja alikusanya wasanii wenzake akawaambia kuwa mimi ni malaya, nimempora mume wake kisa tu alisikia napiga stori na jamaa huyo, bila kuchunguza akaanza kueneza maneno bila kujua nina ndoa yangu.

“Khaa! Nimetokea kumchukia sana Wolper, ni mlugaluga na mnafiki. Ukweli ni kwamba mimi ndiye niliyemtoa Wolper, alikuwa akiitwa Pacha wa Irene na kwenye filamu ya Oprah alifananishwa na mimi ndiyo akatoka.

“Ukweli mimi sifanani na Wolper hata kidogo na sitaki kufananishwa naye kwani hatufanani tabia.
“Mimi nikishasema basi ni basi, siwezi kukaa meza moja na Wolper.”

HUYU NDIYE WOLPER
Baada ya akina Wema kutema ‘mbofumbofu’ kideoni, Ijumaa lilimtafuta Wolper aliyedaiwa kujipanga kujibu mapigo ambapo alifunguka juu ya Wema na Uwoya:
“Uwoya anaficha ukweli, siyo siri, alinichukulia mchumba’ngu na kuniharibia maisha yangu. Kwanza sisumbuki na Wema coz namuona…(neno kali).”

CHANZO CHA YOTE NI WANAUME
Katika mtiti huo, uchunguzi wa Ijumaa ulibaini kuwa pamoja na Wema kupindisha maelezo akidai kumchukia Wolper kwa kumdhalilisha gazetini kuwa hana kitanda wala pakuishi hivyo aende amchezeshe filamu ampe fedha, nyuma yake kuna kisa cha mwanaume (Diamond).

Kwa upande wa Uwoya, pia inadaiwa kuwa sosi ya yote ni mwanaume (Jeff) ambaye anatamkwa kupenda kudandia mapenzi ya mastaa wa kike Bongo.