Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani ambaye pia ni Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Alex Malasusa akisalimia watoto nje ya lango kuu la Kanisa la Azania Front baada ya kumalizika kwa Ibada ya Krismasi jijini Dar es Salaam. (Picha na Mohamed Mambo).

MAASKOFU WASEMA ``VIONGOZI WAACHE TAMAA``

MAASKOFU nchini wametumia ibada za mkesha na Sikukuu ya Krismasi jana, kuwataka viongozi wa umma nchini kuacha ubinafsi, tamaa na kujilimbikizia mali kwa sababu tabia
hizo zinaweza kuliingiza taifa katika machafuko.

Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Tabora, Mhashamu Paul Ruzoka, amesema tabia hizo zimekuwa ikiwafanya wananchi wakate tamaa, kwa sababu inawasababisha viongozi wenye tamaa kushindwa kufuata maadili ya utumishi wa umma na hivyo kugeuka kama maadui wao kwani wanashindwa kutenda haki.

Alisema ni vyema sasa tukarejea katika misingi ya maadili aliyoianzisha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere iliyojenga taifa lenye umoja na usawa na kuwafanya Watanzania kujiona watu kutoka sehemu moja.

Alilaumu kufutwa kwa Azimio la Arusha ambalo alisema uwepo wake ungesaidia kuimarika kwa maadili ya viongozi na kupunguza tamaa na ushindani wa viongozi kumiliki mali na kuwasahau wananchi.
Akihubiri katika Ibada ya Krismasi Kitaifa jana katika Kanisa la Mtakatifu Theresia Mtoto wa Yesu mjini Tabora, Askofu Ruzoka, pia aliwataka viongozi kuhakikisha kuwa utekelezwaji wa sera ya Kilimo Kwanza nchini, haiathiri wananchi na kuwaacha bila ya kuwa na ardhi.

Alisema sera hiyo sasa inahimiza uwepo wa wawekezaji na hivyo kuwepo kwa hatari ya Watanzania kuwa watumwa katika ardhi yao au kutumikishwa katika mfumo wa manamba, ambapo aliuliza wakishachukua ardhi, kuna nini tena kitakachobakia.

Akizungumzia athari za kutokuwepo kwa Azimio la Arusha, alisema ni pamoja na kuwepo kwa
mbio za utajiri baina ya viongozi, kutofuatwa kwa maadili ya uongozi, kutokuwa na miiko, kuongezeka kwa posho katika vikao vingi na kuibuka kwa mrabaha katika kazi mbalimbali za kiserikali na kukithiri kwa tamaa.

Naye Mchungaji Mwaipopo wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Usharika wa Kanisa Kuu, Dodoma Mjini, amewataka wabunge kuacha ubinafsi wa kujilimbikizia posho kwani hali ngumu ipo kwa kila Mtanzania.

Mchungaji Mwaipopo alisema hali ya kumcha Mungu imewakimbia viongozi wengi mbalimbali nchini ambao wanaonekana kujali maslahi yao binafsi kuliko kujali wananchi walio wengi.



Alisema anashukuru viongozi kutambua maisha ya Dodoma yako juu kiasi kwamba hawawezi kuishi kwa posho ya Sh 70,000 kwa siku.

Alisema maisha ni magumu Dodoma kwa kila mtu si kwa wabunge tu, iweje kundi hilo dogo
lisikilizwe je wananchi wakimbilie wapi?
“Kuna kukata tamaa kila kona, kuna majanga ya kutisha, mafuriko, ajali sasa hivi kifo kimetawala duniani kote.” Alisema Mchungaji Mwaipopo.

Naye Askofu wa Dayosisi ya Central Tanganyika, Godfrey Mhogole wa Kanisa la Anglikana, amemlalamikia Ofisa Elimu wa Mkoa wa Dodoma kwa kufuta matokeo ya watoto waliofaulu
darasa la saba mwaka huu.

Alisema iwapo ofisa huyo hataondolewa, yuko tayari kumshitaki kwa kiongozi wa nchi. Alisema kuna haja kwa Ofisa Elimu Mkoa kuangalia kwa kina suala hili kwani halileti picha nzuri katika sura ya elimu nchini.

Alisema katika Shule ya Msingi ya Bishop Stuart DCT iliyopo Msalato mwaka huu walifaulu wanafunzi wanne tu, hali iliyoleta mshtuko kwao.

Alisema kwa miaka mingi shule hiyo imekuwa ikifaulisha sana wanafunzi, lakini anashangaa mwaka huu wanafunzi waliofaulu wamefutiwa matokeo.

Aidha, Askofu Telesphor Mkude wa Jimbo Katoliki la Morogoro, amemwomba Rais Jakaya Kikwete kuwawajibisha watendaji wa Serikali ‘wachakachuaji’ wanaohusika kwa namna moja ama nyingine kuruhusu wananchi kujenga makazi mabondeni na waliosababisha udanganyifu katika mtihani wa Darasa la Saba.

“Yaliyotokea kwa wenzetu walioathiriwa na mafuriko baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es Salaam, ni janga kubwa sana na wanahitaji kusaidiwa na Watanzania wote, lakini ninaunga
mkono kauli ya Rais Kikwete aliyowaambia waliojenga mabondeni wahame,” alisema Askofu Mkude.

“Binafsi ninamwomba Rais awawajibishe watumishi wa Serikali waliochangia maafa haya kwa vile wamechakachua kwa kujipatia fedha kupitia ugawaji wa viwanja na kusambaza huduma nyingine zilizowaingizia mapato kama umeme na maji…nao wawajibishwe,” alisisitiza Askofu Mkude.

°Kuhusu udanganyifu wa mtihani wa Darasa la Saba iliyosababisha wanafunzi wengi kufutiwa matokeo yao, Askofu Mkude aliipongeza Serikali kwa kuchukua hatua ya kuwafutia matokeo wanafunzi hao.

Kwa mujibu wa Askofu huyo, ni aibu kwa mwanafunzi kufaulu mtihani kwa njia ya udanganyifu, kuiba mtihani kwani jambo hilo linasababisha taifa kuwa vijana wasiokuwa
na elimu inayokidhi mahitaji.

Kwa upande wa Katiba mpya, Askofu Mkude alipongeza uamuzi wa kuandikwa kwa Katiba hiyo ambayo itatokana na matakwa ya Watanzania wote.

Aidha, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ameonya kile alichosema ni baadhi ya watu kuwageuzia na kuwatungia maneno watu wanaojitokeza kupinga dawa za kulevya.

Amesisitiza kuwa dawa za kulevya ni janga la taifa ambalo mapambano dhidi yake hayapaswi
kubezwa na mtu yeyote kutokana na namna zinavyoathiri vijana na pia watu wazima.

Habari hii imeandikwa na Lucas Raphael, Sifa Lubasi, John Nditi, na Stella Nyemenohi.

°Kuhusu udanganyifu wa mtihani wa Darasa la Saba iliyosababisha wanafunzi wengi kufutiwa matokeo yao, Askofu Mkude aliipongeza Serikali kwa kuchukua hatua ya kuwafutia matokeo wanafunzi hao.

Kwa mujibu wa Askofu huyo, ni aibu kwa mwanafunzi kufaulu mtihani kwa njia ya udanganyifu, kuiba mtihani kwani jambo hilo linasababisha taifa kuwa vijana wasiokuwa
na elimu inayokidhi mahitaji.

Kwa upande wa Katiba mpya, Askofu Mkude alipongeza uamuzi wa kuandikwa kwa Katiba hiyo ambayo itatokana na matakwa ya Watanzania wote.

Aidha, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo ameonya kile alichosema ni baadhi ya watu kuwageuzia na kuwatungia maneno watu wanaojitokeza kupinga dawa za kulevya.

Amesisitiza kuwa dawa za kulevya ni janga la taifa ambalo mapambano dhidi yake hayapaswi
kubezwa na mtu yeyote kutokana na namna zinavyoathiri vijana na pia watu wazima.

Habari hii imeandikwa na Lucas Raphael, Sifa Lubasi, John Nditi, na Stella Nyemenohi.

                                    CHANZO CHA HABARI NI HAPA