MWANAMKE mmoja mkazi wa Bomani mjini hapa ambaye ni fundi wa kushona, anashikiliwa na jeshi la polisi kwa kosa la kukutwa na mtambo na vifaa vya kutengenezea noti bandia.

Hayo yamethibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Rukwa, Isuto Mantage aliyemtaja mtuhumiwa kuwa ni Dafrosa Ramadhani (30).

Alikamatwa usiku wa kuamkia jana, majira ya saa tano.

Akifafanua, Kamanda Mantage alisema kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo kuliwezekana baada
ya polisi kupata taarifa za siri na baada ya kupekuliwa nyumbani kwake, alikutwa na mabunda
manne ya karatasi zilizokatwa mfano wa noti.

Kwa mujibu wa Mantage, mama huyo pia alikutwa na mabunda mengine manne yenye
karatasi nyeusi mfano wa dola ya Kimarekani.

Ilidaiwa kuwa kila bunda moja la karatasi nyeusi lilikuwa limewekewa alama kuonesha kuna dola za Kimarekani 100,000, sawa na Sh milioni 170.

Mantage aliendelea kuorodhesha vifaa vingine kuwa ni pamoja na kasha moja lenye chupa nne
zenye dawa ya kusafishia fedha hizo za Marekani na chupa nne tupu za dawa hizo.





Pia mwanamke huyo alitajwa kukutwa na makasha mawili na paketi kumi za dawa ambazo hazijajulikana zikidhaniwa kutumika katika shughuli hiyo ya kutengeneza noti bandia pia alikutwa na raba na gundi ya karatasi.

“Mtuhumiwa huyu alipohojiwa alidai kuwa vifaa hivyo ni mali ya mume wake aitwaye Filicon Kaembi ambaye alifanikiwa kutoroka kabla ya kukamatwa na polisi...bado tunaendelea na msako wa kumtafuta,” alisema Mantage.

Alidai kuwa mtuhumiwa bado anaendelea kuhojiwa na polisi ambapo atafikishwa mahakamani
mara tu uchunguzi wa awali utakapokamilika.



Picha haihusiani na maelezo.