TAFAKURI YANGU

Hizo picha hapo juu ni moja ya sehemu ya  mji wa Den haag ambao una pilika pilika nyingi sana(Den haag hollandspoor).
Katika hiyo barabara kuna shuguli nyingi sana zinafanyika kama mnavyoona, kuna matram,magari,baiskeli pamoja na wapita njia na ni kituo kimojawapo kikubwa cha treni.

Pamoja na hayo yote cha kufurahisha hapa ni kwamba katika miaka yangu nane niliyoshi mji huu sijawahi kuona wala kusikia ajali katika eneo hili pamoja na pilika pilika zote za hapo.
Hii inatokana na usimamizi mzuri wa serikali juu ya matumizi ya barabara na mazingira kwa ujumla,kwa kweli serikali za wezentu zina stahili pongezi na wananchi wake pia kwa utiifu.Kwanza wenzetu hawana leseni za kununua na Holland ni nchi inayoongoza kwa kuwa makini katika utoaji wake wa leseni hapa ulaya na ndio maana ajali za barabarani ni chache mno.


Kingine  ni kwamba wanatilia mkazo kufuatilia sheria za barabarani na kila atayekiuka sheria ya barabarani basi atapigwa faini kali ambayo huwezi kuikwepa  na utakapochelewesha ndio inazidi na hizi sheria hujumuisha watu wote wanaotumia barabara kuanzia wapita kwa miguu,waendesha baiskeli,madereva wa magari na matram ambao wao huwa makini maradufu ili kuepuka ajali mbaya ambazo zinaweza kutokea endapo kosa dogo litatokea kwani tram ni kama treni inayopita barabarani kwa hiyo madhara yake yatakuwa ni makubwa sana.


Vilevile kama utaangalia hapo kwenye picha vizuri,pamoja na pilika pilika nyingi iliyokuwepo sehemu hiyo hakuna foleni za magari na huo ndio utaratibu wa wenzetu wa kisayansi.
Najaribu kufananisha na nyumbani naona hayo yote niliyoeleza hapo ni kinyume chake na zaidi,sina haja ya kuyazungumzia kwani tunaweza kumaliza kurasa zote  za humu ndani na kuondoa maana nzima ya blog na ikawa bado hatujamaliza, nafikiri karibu wote tunajua.

Na kwa hayo machache hapo juu naweza kusema hii ndio Tafakuri ya Leo.(Na Shekh Hija wa Den Haag- Holland).