Na Christina Gauluhanga, Dar es Salaam
VILIO na simanzi vilitawala jana kwa wananchi wa Ukonga Mzambarauni, jijini Dar es Salaam, baada ya bwana harusi mtarajiwa, Rashid Hamad kufariki ghafla wakati wa mkesha wa sherehe yake.

Tukio hilo ambalo limewahuzunisha ndugu na majirani wa familia hiyo, lilitokea jana saa 8 usiku wakati wana familia hao na majirani wakiendelea kuserebuka na rusha roho nyumbani kwa bwanaharusi huyo.

Akizungumza na MTANZANIA jana nyumbani kwao Mzambarauni baba mkubwa wa marehemu, Ally Khatibu alisema, wamesikitishwa na kifo cha ghafla cha kijana wao.

Alisema kifo cha mtoto wake ambaye ni kondakta wa daladala, kimekuwa cha ghafla mno kwani kimetokea wakati familia zikiendelea na taratibu za kusherehekea harusi yake.

Kwa mujibu wa Khatibu, ndoa ya kijana huyo ilipangwa kufungwa jana saa saba mchana na kwamba taratibu zote zilikuwa zimekamilika.

“Tulikuwa na marehemu mchana kutwa alikuwa hajalalamika kuumwa kitu chochote na usiku wote huo alikuwa akicheza na wenzake ambao walikuja kumuunga mkono kwenye mkesha.

“Tunashangaa mara baada ya kutaka kwenda kuoga kutokana na uchovu aliokuwa nao ghafla alipiga mayowe ya kuomba msaada akidai anakufa.

“Kutokana na mayowe hayo ndugu waliokuwepo waliingia ndani, ndipo tulipokuta Rashid amekata kauli ghafla,” alisema.

Khatibu alisema kijana huyo kutokana na hali hiyo alikimbizwa katika Zahanati ya MICO iliyopo Mzambarauni kwa ajili ya kuokoa maisha yake.

Alisema baada ya kufika Mico wahudumu hawakuweza kufanya lolote na kushauri kijana huyo awahishwe Hospitali ya FFU, Ukonga na badaaye kupelekwa Amana kwa madai kuwa hali yake haikuwa nzuri.

Baada ya kufika hospitali ya Amana wauguzi walimuingiza wodini mgonjwa huyo na ndipo familia hiyo ilipotaarifiwa kuwa mgonjwa wao alikuwa amekwishafariki dunia.

“Kwa kweli hatukuamini macho yetu na hadi sasa hatuelewi kilichomsibu kijana wetu kama ni shoti ya umeme au laa,” alisema Khatibu.

Alisema mwili wa marehemu huyo unatarajiwa kusafirishwa kwenda Kimanzichana, wilayani Mkuranga kwa ajili ya mazishi.
Chanzo: Mtanzania