Wakati majeshi ya Kenya na Somalia yanakaribia mji wa Kismayo, sehemu ya mkakati wa miaka mingi wa Kenya karibu kukamilia.
Mpango wa kuwa na eneo la salama la kuzunguka mipaka ya Kenya karibu kukamilia:

Kwa miaka mingi, imekuwapo siri ambayo siyo siri tena, kwamba Kenya itapenda kuona taifa salama linaundwa nje ya mpaka wake na Somalia.

Huo ndio unaitwa makakati au mradi wa Jubaland.

Mpango huo unaungwa mkono na Wasomali wa Kenya.

Kati ya hao ni Waziri wa Ulinzi wa Kenya, Mohamed Yusuf Haji na mwanawe, Nuradin Yusuf, afisa wa ujasusi katika jeshi la Kenya.


Wote hao wanatokana na koo za Ogaden, ambazo zimetapakaa kaskazini mwa Kenya, kusini mwa Somalia na katika jimbo la Wasomali mashariki mwa Ethiopia.
Lakini kulikuwa na tatizo moja kubwa katika kuunda Jubaland, nalo ni upinzani wa Ethiopia.

Tangu miaka ya 1980, Waethiopia wamekuwa wakipigana vita na kundi la ONLF, wapiganaji wa jimbo la Ogaden.

Serikali ya Ethiopia inapinga kabisa wazo hilo la kuwa na Jubaland, ikiwa itaruhusu ONLF kuwa na kambi kupigana na majeshi ya Ethiopia.

Kwa hivo awali mwezi huu Waziri wa Ulinzi wa Kenya alipatanisha na kuleta makubaliano baina ya wapiganaji hao na serikali ya Ethiopia.

Kwa hivyo kikwazo cha mwisho dhidi ya mradi wa Jubaland sasa kimeondoka, na hivo kusukuma shambulio la hivi sasa dhidi ya Kismayo.

Tatizo moja limebaki: watu wa Kismayo siyo wa koo za Ogaden, na hiyo ndio sababu moja watu waliunga mkono al-Shabaab.

Kenya itabidi kusikiliza wasiwasi wao, ikiwa inataka kufanikiwa kukamilisha mradi wa Jubaland.