Vitendo vya hivi karibuni vya mauaji na utesaji wa waandishi wa habari nchini, vimechafua jina la Tanzania baada ya taarifa hizo kusambaa katika nchi mbalimbali duniani.
Tatizo la usalama wa waandishi wa habari nchini, lilikuwa ndiyo ajenda kuu katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, yaliyofanyika kwa siku mbili mjini Arusha, yakiwakusanya wanahabari kutoka nchi za Afrika Mashariki.
Maadhimisho hayo ya Mei 3 na 4 mwaka huu, yalizinduliwa kwa machapisho kadhaa likiwamo toleo la 19 liitwalo “So this is democracy?” (Kwa hiyo hii ndiyo demokrasia?), lilitolewa na Taasisi ya Vyombo vya Habari Kusini mwa Afrika (Misa).
Kitabu hicho ambacho ni zao la nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), kinaitaja Tanzania kwamba ni kinara wa vitendo vya kuteka, kushambulia na kuuawa kwa waandishi wa habari na wanaharakati katika kipindi cha mwaka jana na miezi ya mwanzo ya mwaka huu.

Tukio la mauaji ya aliyekuwa mwandishi wa habari wa Kituo cha Televisheni cha Channel Ten, Daudi Mwangosi linatajwa kuwa moja ya matukio mabaya dhidi ya uhuru wa habari yaliyotokea mwaka jana katika Ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Afrika.

Jalada la nje na ukurasa wa kwanza wa kitabu hicho imepambwa na picha ya askari polisi wanaomshambulia marehemu Mwangosi kwa kipigo, muda mfupi kabla ya kulipuliwa kwa bomu la kishindo la kutoa machozi ambalo lilisambaratisha baadhi ya viungo vyake na hatimaye, kifo chake.
Kitabu hicho cha kurasa 258 pia kimetumia maelezo ya awali kutaja tukio la kushambuliwa kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Absalom Kibanda kama mifano ya matukio mabaya yaliyowakumba waandishi wa habari nchini.

Katika utangulizi wa kitabu hicho, Mkurugenzi wa Kanda wa Misa-Tan, Zoe Titus ametoa mifano ya matukio ya Tanzania kwamba ni uthibitisho kwamba taasisi yake ilifanya makosa katika miaka ya nyuma kutoa taarifa zinazoeleza kwamba matukio ya kushambuliwa kwa waandishi wa habari yamekuwa yakipungua.

“Mwaka 2012 umekuwa mwaka wenye changamoto kubwa kutokana na kurejea kwa matukio ya kushambuliwa kwa waandishi wa habari, tunaweza kusema tulifanya makosa kusema kwamba mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari yanapungua katika nchi zetu,” anasema Titus katika maelezo yake.

Maelezo mengine kuhusu Tanzania yanapatikana kuanzia ukurasa wa 144 hadi 150 ambapo hali halisi ya uhuru wa habari, kukusanyika na kujieleza imezungumziwa, huku sheria mbaya ikiwemo ile ya magazeti ya mwaka 1976 zikitajwa kama vikwazo.

Mashtaka ya jinai kwa makosa yanayotokana na habari zinazochapishwa au kutangazwa kwenye vyombo vya habari ikiwemo ile inayomkabili Kibanda na aliyekuwa Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mwananchi Communications Ltd, Theophil Makunga, ni miongoni mwa vikwazo kwa uhuru wa habari na kujieleza vinavyotajwa kwenye kitabu hicho.Kifo chenye utata cha mwandishi wa Kituo cha Redio Kwezira cha Wilaya ya Kibondo mkoani Kigoma, Issa Ngumba na lile la kujeruhiwa kwa kupigwa risasi kwa mwandishi Shaban Matutu wa gazeti la Tanzania Daima, pia yametajwa na kuhusishwa na kazi zao ingawa hadi sasa haijathibitika.
Kufungiwa kwa gazeti la MwanaHalisi pia kumetajwa kuwa mifano ya ukiukwaji wa uhuru wa bahari na matumizi ya sheria mbaya inayotekelezwa na dola, kukandamiza haki ya kutafuta na kupasha habari inayolindwa na kifungu cha 18 cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano.

Hata hivyo, Tanzania kwa mujibu wa kitabu hicho ni miongoni mwa nchi zenye idadi kubwa ya magazeti, vituo vya redio na televisheni vilivyosajiliwa, kwa kusajili magazeti 706, vituo 59 vya redio na 28 vya televisheni.

Kitabu hicho kimepongeza juhudi za kutatua migogoro kuhusiana na habari nchini zinazofanywa na Baraza la Habari (MCT) na wadau wengine.