Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya.PICHA|MAKTABA

Mwanga.
Waziri Mkuu mstaafu, Cleopa Msuya amemshauri Rais Jakaya Kikwete kupuuza matatizo madogomadogo yanayojitokeza katika Bunge Maalumu la Katiba badala yake asimamie uamuzi ya Bunge hilo ili kupata Katiba ambayo itaongoza nchi kwa amani. Msuya alisema hayo mbele ya Rais Kikwete jana wilayani Mwanga, Kilimanjaro wakati wa hafla ya kumuaga baada ya kung’atuka katika shughuli za kisiasa, iliyoandaliwa na CCM wilayani hapa. “Majibizano
yanayotokea huko Dodoma kwa sasa katika mchakato wa Katiba yasikukatishe tamaa, simamia uamuzi sahihi ambao utalipeleka Taifa kwenye amani na utulivu,” alisema Msuya.

Pia aliishauri CCM kuhakikisha inarudi chini na kuwa karibu na wananchi, ili kufanikiwa katika malengo yake na kutoa mahitaji kwa wananchi pale yanapohitajika.“Hivi karibuni tumeshuhudia viongozi wakitafuta uongozi kwa kutoa rushwa ili waingie madarakani, ni vyema viongozi wakachaguliwa kwa hiari na siyo kwa kutumia fedha,” alisema Msuya.Alisema viongozi wa namna hiyo ndiyo wanaolipeleka taifa pabaya na hatimaye kuleta mkanganyiko katika chama hasa nyakati za uchaguzi. Alimpongeza Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana kwa kujituma katika kukihudumia chama hicho kiasi cha wananchi wengi kurudisha imani. Akihutubia katika hafla hiyo, Rais Kikwete alisema katika miaka yake 29 ya kukihudumia chama na Serikali, Mzee Msuya amewaachia Watanzania mambo mengi ya kuigwa.Alisema kitendo cha chama kumuaga na kuelezea wasifu wake, ni heshima ya kipekee ambayo wamempa kutokana na kazi nzuri alizofanya katika Serikali na Taifa kwa ujumla.“Mzee Msuya naomba muda huu unaokwenda kuungana na wazee wenzako huko Usangi, uutumie kuandika kitabu ambacho utaachia Taifa kama wasia wako, maana wewe unaifahamu hii nchi vizuri,” alisema Rais Kikwete.