Mh. Edward Lowassa.
Mh. Bernard Membe.
Mh. Stephen Wasira.
Mh. January Makamba.
Mh. William Ngereja.
Mh. Fredrick Sumaye.
Dodoma. Mpambano mkali wa kuwania nafasi ya kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya CCM sasa umeanza rasmi baada ya Kamati Kuu ya chama hicho tawala kuwaweka huru makada sita waliokuwa wamefungiwa kwa takriban miezi 17 kwa makosa ya kukiuka kanuni za uchaguzi.
Kufunguliwa kwa makada hao, ambao baadhi yao wanapewa nafasi kubwa ya kupitishwa na chama hicho, kumekuja wakati CCM ikikabiliwa na tishio la kutokea mgawanyiko mkubwa, hasa kutokana na baadhi ya kambi kuituhumu sekretarieti kuwa inabagua baadhi ya wagombea.
Makada waliofungiwa tangu Februari, 2014 kwa kosa la kuanza kampeni mapema ni mawaziri wakuu wa zamani, Frederick Sumaye na Edward Lowassa, ambaye kwa sasa ni mbunge wa Monduli.
Wengine ni Bernard Membe, ambaye ni Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Steven Wasira (Waziri wa Kilimo na Chakula), January Makamba (Naibu Waziri wa Sayansi na Teknolojia), na mbunge wa Sengerema, William Ngeleja.
Baadhi ya wanachama wa CCM, hasa wajumbe wa Halmashauri Kuu, walianza kumiminika nyumbani kwa makada hao mara baada ya kupata taarifa za kuondolewa kwa adhabu hiyo, wengi wakionekana kwenda kumpongeza Lowassa.
Kufunguliwa kwa makada hao ni mwanzo wa kinyang’anyiro kikali cha kuwania kumrithi Jakaya Mrisho Kikwete kwenye nafasi ya urais na mwenyekiti wa chama hicho kikongwe na dalili zote za kuwapo kwa vita kali zilianza mara moja jana baada ya kutangazwa kwa uamuzi huo.
Makamba: Safari ya ushindi
“Nimefurahishwa na uamuzi wa Kamati Kuu. Safari ya ushindi sasa inaanza,” alisema Makamba alipohojiwa kuhusu tamko hilo la Kamati Kuu.
“Sijashangaa hata kidogo (kusikia uamuzi huo) kwa kuwa sijawahi kukiuka maadili ya chama. Sasa nasubiri muda wa kampeni kutangazwa ili nianze kufanya hivyo kwa kuzingatia kanuni za chama kwa sababu najua wakati wa mchujo wa wagombea, CCM itaangalia tena jambo hili.”
Ngeleja: Nasubiri muda
Ngeleja, ambaye alikuwa Waziri wa Nishati na Madini, aliishukuru Kamati Kuu kwa kufikia uamuzi huo akisema imezingatia misingi yote ya haki na kwamba kilichobaki ni kusubiri muda wa kampeni.
“Hatua inayofuata ni kuhakikisha kwamba nafuata kanuni, taratibu na miongozo ya chama katika kugombea nafasi nitakayoiomba,” alisema mbunge huyo wa Sengerema.
CHANZO NA MWANANCHI