Mtu mmoja apigwa risasi Bujumbura
Habari kutoka Burundi zinasema kuwa mtu mmoja amepigwa risasi na kuuawa katika mji mkuu wa Bujumbura.
Mtu huyo alikuwa miongoni mwa waandamanaji wanaopinga hatua ya rais Pierre Nkurunziza kugombea urais kwa awamu ya tatu.
Walioshuhudia wanasema kuwa polisi walimpiga mwandamanaji huyo risasi mgongoni wakiwa katika eneo la Musaga linalotazamwa kama ngome ya upinzani.

Waandamanaji walijaribu kufika katikati mwa jiji la Bujumbura lakini walitimuliwa kwa mabomu ya moshi wa kutoa machozi.
Rais wa Burundi, Pierre Nkurunziza, amewaomba zaidi ya raia laki moja na hamsini waliokimbia ghasia nchini humo katika majuma kadhaa yaliyopita, warejee nyumbani.
Katika hotuba kwenye runinga ya taifa, amesema kuwa asilimia tisini na tisa nukta tisa ya Burundi ina amani.
Anasema kuwa hakuna mtu yeyote anayetaka kufufua taharuki ya kikabila.
Rais Nkurunziza amewataka raia wa Burundi waliotoroka warejee nyumbani kwani kuna amani
Muda mchache baadaye rais Nkurunziza alionekana akicheza mpira na maswahiba wake wa karibu licha ya maaandamano yanayoendelea mjini Bujumbura.
Kumekuwa na hali ya taharuki mjini Bujumbura haswa kutokea jumatano iliyopita baada ya jaribio la mapinduzi dhidi ya rais Nkurunziza
Rais Nkurunziza amehitimu kama kocha wa kandanda.