KASI ya Rais John Magufuli imeendelea kutikisa idara na taasisi mbalimbali za serikali kutokana na mchakamchaka miongoni mwa watendaji na wasimamizi wanaoendelea kuasa watumishi walio chini yao, kutii falsafa ya ‘Hapa Kazi Tu’ vinginevyo watajiondoa kwenye mfumo.
Ari ya uwajibikaji imeonekana kutawala kwenye taasisi mbalimbali za serikali zikiwemo halmashauri ambako baadhi ya watendaji wameweka bayana kutokuwa tayari kugeuzwa mbuzi wa kafara kwa kutowajibika kwa watumishi walio chini yao. Miongoni mwa halmashauri ambazo wakurugenzi wake wamekaririwa wakisema hawako tayari kuadhibiwa kwa kushindwa kusimamia kasi ya Dk Magufuli ni pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Songea Vijijini.

Akizungumza na wakuu wa idara juzi, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Sigsbert Kaijage, aliwataka wafanyakazi kuhakikisha wanakwenda na kasi ya Rais Magufuli chini ya kaulimbiu ya ‘Hapa Kazi Tu’ ili kuinua hali ya maisha ya wananchi na uchumi wa wilaya kwa ujumla. “Mimi sikubali kugeuzwa mbuzi wa kafara kwa niaba yenu.
Nahitaji kila mmoja kutekeleza wajibu wake na kama kuna mtu anaona hataki kufanya kazi katika halmashauri hii kutokana na maslahi, basi ni vizuri akatafute maeneo mengine, lakini siyo kuendelea kung’ang’ania huku ukishindwa kuleta tija mahali pa kazi,” alisema Kaijage.
Licha ya wakuu wa taasisi mbalimbali kuandaa vikao maalumu kwa ajili ya kuwasilisha maagizo ya rais kwa watumishi walio chini yao, vile vile katika vikao au hafla zinazowakutanisha na watumishi wa chini yao, wamekuwa wakisisitiza umuhimu wa kubadilisha mfumo na kuondokana na kufanya kazi kwa mazoea.
Juzi kwenye hafla ya kumuaga aliyekuwa Ofisa Tarafa ya Namanyere, Nimrod Kaishozi ambaye amestaafu kisheria, Mkuu wa Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa, Idd Kimanta aliendelea kutumia nafasi hiyo kuhimiza umuhimu wa watumishi kubadilika na kuendana na kasi ya Magufuli.
Kimanta alisema mtumishi atakayeshindwa kuendana na ‘Hapa ni Kazi Tu’, atafute mlango wa kutokea haraka iwezekanavyo. Alikiri kuwapo watumishi ambao ni wagumu kuendana na mabadiliko huku akiwahadharisha dhidi ya kufanya kazi kwa mazoea. “Falsafa ya Rais Magufuli na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa haizungumzwi tu, bali inakwenda kwa vitendo… Ambaye anaona kuwa hataendana na kasi hiyo, ni bora akaamua kuondoka mapema kabla ya kuondolewa kazini,” alisema Mkuu wa Wilaya.
Aliwaonya wanaoendekeza itikadi za kisiasa akisema kitakachofuata ni hatua kali za kisheria kuchukuliwa dhidi yao vinginevyo, waamue mapema kuacha kazi. Alisema ameshatoa maelekezo kwa watumishi wote wa Serikali kujipambanua upya. “Inasikitisha kuona baadhi yao wameendekeza siasa na kuacha mambo ya msingi ya kuwatumikia wananchi kama ilivyo katika miongozo yao ya kiutumishi,” alisema.
Akisisitiza uwajibika, Kimanta aliwaambia kwamba kama ambavyo wengi walimuona ama kumsikia Dk Magufuli akihutubia Bunge la 11, mambo aliyosema alimaanisha utekelezaji na uwajibikaji. Alisisitiza kwamba kama yupo mtu anayeona ni utani, ataanza naye kummaliza.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Fadhili Nkulu, alitoa rai kwa wahitimu wa Chuo cha Uhasibu kilichoko Arusha kutumia taaluma walizopata kwa kuitikia kaulimbi ya ‘Hapa Kazi Tu’. “Nawasihi mkatumie taaluma yenu vizuri, sababu serikali tulionayo ‘sasa ni kazi tu’. Atakayeleta mchezo atakuwa anachezea kibarua chake mwenyewe,” alisema Nkulu aliyekuwa mgeni rasmi katika mahafali ya 17 ya chuo hicho.
Tangu Rais Magufuli alipoapishwa Novemba 5 na kuweka wazi msimamo wake kuhusu uwajibikaji, watumishi serikalini wameendelea kuhadharishwa wakiambiwa atakayeshindwa kuendana na mabadiliko, yuko kwenye hatari ya kupoteza kazi. Makatibu wakuu wa wizara mbalimbali wameendelea kukutana na taasisi zilizo chini yao kueleza maagizo ya rais kwa ajili ya utekelezaji.
Hotuba yake bungeni iliyopigilia msumari msimamo wake, imeendelea kuibua mjadala mkubwa kwenye majukwaa mbalimbali, ikiwemo mitandao ya kijamii na vyombo vya habari. Wachangiaji wengi wameasa watendaji wa umma wanapaswa kutekeleza maagizo ya rais vinginevyo, wapo watakaopoteza ajira. Wasomi, wanasiasa na viongozi wa sekta mbalimbali binafsi, wameelezea hotuba yake kuwa ya kihistoria inayoonesha dhamira ya kweli kwa nchi.
Maeneo ambayo rais aliyatilia mkazo katika hotuba yake, ni pamoja na ukusanyaji wa mapato ambao alisema umekuwa chini ya makadirio kutokana na sababu mbalimbali. Udhibiti wa safari zote za nje ya nchi zisizo za lazima kwa ajili ya kupunguza matumizi, ni eneo ambalo liliibua mjadala mkubwa hususani baada ya rais kutoa takwimu za baadhi ya taasisi za serikali zilizoongoza kwa kutumia fedha nyingi kutokana na safari hizo.
Miongoni mwa wasomi waliokaririwa na gazeti hili, ni Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk Benson Bana aliyesema watendaji wa umma wanapaswa kutekeleza maagizo huku akisema sasa utakuwa mwisho wa kufanya kazi kwa mazoea. Kwa upande wake, Mbunge wa Kigoma Mjini, Kabwe Zitto (ACT Wazalendo), alisema mtu atakayempinga Magufuli, analinda mafisadi na ana maslahi nao.