KATIBU Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Sifuni Mchome, amesema wizara yake inaandaa mwongozo utakaotoa maelekezo juu ya muundo, mfumo na utaratibu nyumbufu utakaohakikisha kuwa ifikapo Januari mwakani, elimu ya msingi inatolewa bila malipo.
Profesa Mchome aliyasema hayo juzi jioni katika kikao na watendaji wakuu wa taasisi zote na vyuo vilivyopo chini ya wizara yake katika kuhakikisha wanatekeleza maagizo ya Serikali ya Awamu ya Tano. Chini ya Rais John Magufuli, Serikali imetangaza kuwa kuanzia mwakani itatoa elimu bure kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha nne.

Profesa Mchome alisisitiza juu ya utekelezaji wa kutoa elimu bure bila kuathiri ubora wa elimu itakayotolewa na kuziagiza taasisi zinazohusika pamoja na walimu kushughulikia kero zao katika ngazi mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa nyumba za walimu.
Alisema wizara yake inatarajia kuongeza uandikishwaji wa watoto wa awali kutoka asilimia 45 mwakani hadi asilimia 100 ifikapo mwaka 2020. Katika kikao hicho ambacho pia kilijadili mwelekeo wa Sera na Mipango ya Elimu katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Tano, Profesa Mchome alisema wizara inajipanga kuhuisha taratibu za kujiunga na taasisi zinazotoa elimu msingi na mafunzo katika ngazi mbalimbali.
Profesa Mchome alitoa vipaumbele elekezi 20 vya utekelezaji katika kuboresha sera na mipango ya elimu kwa kipindi cha miaka mitano kutoka 2015 hadi 2020. “Wizara ina mpango wa kuandaa mfumo, muundo na taratibu nyumbufu za kutoa elimu ya awali na elimu ya msingi bila malipo ili kuongeza uandikishwaji wa watoto wa awali kutoka asilimia 45 mwaka 2015 hadi asilimia 100 ifikapo mwaka 2020,” alisema Profesa Mchome.
Aidha, Profesa Mchome alisisitiza kuhuisha sifa na kutambua sifa zinazohitajika katika mifumo na taasisi tofauti ili kuongeza udahili ili asilimia 20 ya wahitimu wa elimu ya msingi wawe wakijiunga na elimu ya sekondari huku asilimia 80 wakiendelea na mafunzo ya ufundi.
Alisema lengo la mpango huo ni kuhakikisha kuwa asilimia 70 ya wahitimu hao wanaweza kujiajiri na kuajiriwa ili kukidhi mahitaji ya soko hasa ikizingatiwa kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imekusudia kupeleka nchi katika uchumi wa viwanda.
Pia aliziagiza taasisi zilizo chini ya wizara kuhuisha mipango yake kufikia malengo ya uongozi wa Dk Magufuli ikiwemo kuongeza nafasi za wanafunzi kujiunga na taasisi mbalimbali na wakati huo huo ubora wa elimu inayotolewa iwe chachu ya maendeleo.
Alizitaka taasisi hizo na vyuo kuhakikisha kuwa wanaweka msisitizo katika masomo ya sayansi ili kuandaa wanasayansi wa kutosha katika kumudu mahitaji ya soko la uchumi wa viwanda.
Aliviagiza vyuo vya elimu ya juu kukaa pamoja ili kujadili mahitaji ya kitaifa na kuandaa programu zitakazokidhi mahitaji hayo na kuitaka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu kupitia upya vigezo vya utoaji wa mikopo kulingana na vipaumbele vya mahitaji ya soko.