WIZARA ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi imewatahadharisha wananchi kuepuka kujenga katika maeneo ya wazi na kuvamia viwanja, kwani kazi ya bomoabomoa ni endelevu. Kauli hiyo ilitolewa jana Dar es Salaam na Ofisa Habari wa Wizara hiyo, Mboza Lwandiko alipofanya mahojiano na gazeti hili.
Lwandiko alisema ubomoaji uliofanyika katika Wilaya ya Kinondoni mkoani Dar es Salaam hivi karibuni ni ya awali kwani wanaendelea na uhakiki ili kubaini maeneo mengine yaliyovaamiwa na kujengwa bila kufuata taratibu.

Alisema Wizara inasubiri uhakiki wa maeneo ukamilike na kisha itatangaza maeneo yanayopaswa kubomolewa, hivyo wananchi wanapaswa kuepuka kuvamia maeneo ya wazi na kujenga bila kufuata utaratibu ili kuepuka kuja kubomolewa nyumba zao.
“Ubomoaji unatia hasara na unamrudisha mtu nyuma. Tunaomba wananchi wafuate taratibu, wajenge katika maeneo sahihi,” alisema Lwandiko. Aliongeza kuwa ubomoaji wa nyumba hizo zilizojengwa bila kufuata taratibu na zile ambazo zipo katika maeneo ya wazi utafanyika kwa nchi nzima sio kwa Wilaya ya Kinondoni pekee.
“Wahakiki wanapita katika maeneo mbalimbali ya nchi na kuhakiki ili kuendelea kubaini maeneo mengine ili kuhakikisha hakuna uvamizi wala nyumba zilizojengwa bila kufuata taratibu,” alisema Lwandiko.
Hivi karibuni, Wizara ikishirikiana na Wilaya ya Kinondoni iliendesha bomoaboamoa katika wilaya ya Kinondoni ambapo nyumba zaidi ya 20 zilizojengwa bila kufuata taratibu na za watu waliovamia maeneo ya wazi zilibomolewa.