Polisi nchini Ubelgiji wamewakamata washukiwa 16 katika operesheni ya kukabiliana na ugaidi Brussels, lakini mtuhumiwa mkuu wa mashambulio ya Paris Salah Abdeslam bado hajakamatwa.
Polisi walifanya misako 22 katika maeneo mbalimbali Jumapili katika miji ya Brussels na Charleroi, msemaji wa mwendesha mashtaka mkuu wa serikali alisema.
Mji wa Brussels bado umesalia katika hali ya juu zaidi ya tahadhari. Vyuo vikuu, shule na treni vyote vimefungwa.
Watu 130 waliuawa na 350 kujeruhiwa kwenye mashambulio ya Paris yaliyotekelezwa Novemba 13.
Polisi walifyatulia risasi gari moja wakati wa operesheni mtaa wa Molenbeek mjini Brussels, na kujeruhi mshukiwa mmoja ambaye baadaye alikamatwa.
Hakuna silaha zozote zilizopatikana wakati wa misako hiyo ya Jumapili, msemaji wa mwendesha mashtaka mkuu Eric Van Der Sypt aliambia wanahabari.
Serikali ya Ufaransa imesema meli yake ya kubeba ndege za kivita ya Charles de Gaulle itaanza kutumiwa kwenye bahari ya Mediterranean Jumatatu na iko tayari kutumiwa kwa mashambulio dhidi ya IS nchini Syria.
Image copyrightPolicia de Francia
Mji wa Brussels umedhibitiwa na maafisa wa usalama wikendi yote huku polisi wakiendelea kumsaka Abdeslam, ambaye anashukiwa kuwa mhusika mkuu katika amshambulio hayo ya Paris.
Waziri wa masuala ya ndani wa Ubelgiji Jan Jambon amesema hatari iliyoko Ubelgiji haihusiani na Abdeslam pekee.
Mohammed Abdeslam, kakake Brahim Abdeslam aliyejilipua wakati wa mashambulio ya Paris na Salah Abdeslam, alizungumza na runinga ya Ubelgiji na kumhimiza kakake mtoro kujisalimisha.