John Pambalu ambae ni diwani wa Kata ya Butimba (Chadema) akiwasilisha mchango wake katika kikao cha baraza la madiwani Jijini Mwanza.
Na:George Binagi-GB Pazzo
Madiwani wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
Chadema Jijini Mwanza, wamemlalamikia Mstahiki Meya wa Jiji hilo kwa madai ya
kuliongoza kibabe baraza la Madiwani.

Wakizungumza baada ya kikao cha baraza
la Madiwani kilichoketi hii leo, Madiwani hao wamelalamikia kitendo cha
kuzuiliwa kujadili taarifa ya Kamati ya fedha iliyowasilisha katika kikao hicho
kwa madai kwamba jukumu la baraza hilo ni kupitisha taarifa hiyo na si
kuijadili.


Samwel Range ambae ni diwani wa Kata
ya Pamba pamoja na John Pambalu ambae ni diwani wa Kata ya Butimba (Wote
Chadema), wamesema wamesikitishwa kuona kanuni za vikao zikivunjwa huku
madiwani wakinyimwa fursa ya kujadili taarifa ya kamati ya fedha
iliyowasilishwa.

“Tumeshuhudia utawala wa kibabe
ukianza katika halmashauri yetu huku mhe.Mwenyekiti wa kikao (Meya) pamoja na
Mkurugenzi wake wakiamua kutofuata kanuni na kuamua kufuata matakwa yao
binafsi. Tumeletewa taarifa ya kamati ya fedha, wakati wa kujadili tunaambiwa hakuna
sababu ya kuijadili isipokuwa kuipitia na kuiidhinisha taarifa hiyo, kitu
ambacho madiwani wa Chadema na Upinzani tunakilalamikia”. Alisema Pambalu.

Nae Samwel Range amesema “Kamati ya
fedha haina mamlaka ya kuidhinisha chochote ndani ya halmashauri ya Jiji la
Mwanza. Inapaswa ilete taarifa yake na kuileta katika baraza la Madiwani ambapo
sisi tunauwepo wa kuikubali au kuikataa”.

Hata hivyo malalamiko hayo yamepingwa
na James Bwire ambae ndie Mstahiki Meya wa Jiji la Mwanza na diwani wa Kata ya
Mahina (CCM), ambapo amefafanua kwamba malalamiko ya madiwani wa Chadema hayana
msingi wowote ikizingatiwa kwamba taarifa iliyowasilishwa na kamati ya fedha
iliishajadiliwa ndani ya kamati hivyo hakukuwa na umuhimu wa kuijadili tena
ndani ya baraza la madiwani bali kuipokea na kuipitisha.

Baraza la Madiwani Jijini Mwanza linaundwa
na Madiwani 24 na linaongozwa na Chama cha Mapinduzi CCM kwa upande wa Mstahiki
Meya pamoja na Naibu Meya ambapo kuna Madiwani 19 kutoka CCM huku Chama cha
Demokrasia na Maendeleo Chadema kikiwa na Madiwani Watano.



Kutokana na Uwiano huyo, Madiwani wa Chadema
wanalalamika kuburuzwa katika baraza hilo kutokana na uchache wao, madai ambayo
hata hivyo yanapingwa na Madiwani kutoka CCM ambao wanasema suala lolote lenye
maslahi kwa umma linapewa nafasi sawa ndani ya baraza hilo bila kujadi itikadi
za vyama vya siasa. 



Kushoto ni Naibu Meya Jiji la Mwanza, Katikati ni Mstahiki Meya na Kulia ni Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza
Waheshimiwa Madiwani Jijini Mwanza
Waheshimiwa Madiwani Jijini Mwanza
Watendaji wa Idara mbalimbali Jijini Mwanza.