MBUNGE wa Viti Maalumu, Jesca Kishoa (Chadema) amekuwa mbunge wa kwanza wa Bunge la 11, kukumbana na rungu la Kiti cha Spika baada ya kusimamishwa kuhudhuria vikao vitano vya Bunge kwa kusema uongo.
Adhabu hiyo imetolewa na Kiti cha Spika kutokana na mbunge huyo, kushindwa kuthibitisha madai aliyotoa bungeni Februari Mosi, mwaka huu wakati akichangia Mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2016/17.
Mbunge huyo katika kuchangia, alimshutumu Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Harrison Mwakyembe kuhusu ununuzi wa mabehewa, aliyosema yalikuwa feki na yalinunuliwa kwa Sh bilioni 238 na kuingiza taifa kwenye hasara.

Akitoa Mwongozo ulioombwa na Dk Mwakyembe dhidi ya Kishoa siku alipochangia kwa kuthibitisha kwamba hakuna mabehewa feki yaliyonunuliwa na wakati huo, akisema gharama halisi zilizotumika ni Sh bilioni 60 na si Sh bilioni 238 zilizodaiwa, Mwenyekiti wa Bunge, Dk Mary Mwanjelwa alimpa Kishoa siku 14 athibitishe madai hayo.
Hata hivyo, jana akitoa uamuzi, Mwenyekiti wa Bunge, Andrew Chenge alisema hadi jana hapakuwa na ushahidi, uliopokewa kutoka kwa mbunge huyo kuthibitisha kauli yake kuhusu gharama zilizotumika kununua mabehewa. Akitumia Kanuni ya 63 (8), Chenge alimpa nafasi mbunge huyo ya kufuta kauli aliyotoa siku alipochangia.
Lakini mbunge huyo alisema, “lakini niseme tu kwamba sitafuta kauli niliyosema kwa sababu Mwakyembe hajathibitisha.” Kanuni zilizozingatiwa katika uamuzi huo ni ya 63 (6) inayosema: Mbunge anayetakiwa kuthibitisha ukweli wa kauli au usemi au maelezo yake aliyoyatoa bungeni, atawajibika kutoa uthibitisho huo kwa kiwango cha kuliridhisha Bunge, papo hapo au katika muda atakaopewa na Spika kwa ajili ya kufanya hivyo.
Kanuni ya 63 (8) inasema: endapo hadi kufikia mwisho wa muda aliopewa, Mbunge aliyetakiwa kutoa uthibitisho wa ukweli wa kauli au usemi au maelezo yake aliyotoa bungeni atakataa au atashindwa kutoa uthibitisho huo kwa kiwango cha kuridhisha Bunge na kama atakataa kujirekebisha kwa kufuta kauli au usemi au maelezo yake, basi Spika atamwadhibu kwa kumsimamisha mbunge huyo asihudhurie vikao vya Bunge visivyozidi vitano.
Chenge alisema kwa kuwa Kanuni inamtaka amsimamishe kwa siku zisizozidi tano, na kwa kuwa zimebaki siku mbili za mkutano kumalizika, alimsimamisha kuhudhuria vikao viwili; jana na leo.
Baada ya kutoa adhabu hiyo na kumtaka atoke nje, mbunge huyo ambaye ni mke wa aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), aliondoka kwa mwendo wa haraka huku akionesha kujibizana na wabunge, ambapo upande wa upinzani ulikuwa ukimshangilia.
Kutokana na shutuma zilizotolewa kwa Mwakyembe siku hiyo mbunge alipochangia, Mwakyembe alisimama kuhusu utaratibu na kuithibitishia Kamati ya Mipango kwamba yalinunuliwa mabehewa 204 na serikali ilitumia Sh bilioni 60. Alimtaka Kishoa athibitishie Bunge kuhusu madai yake.
Hata hivyo, yalitokea malumbano ambayo Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Waziri Jenista Mhagama waliingilia kati kutoa ufafanuzi kuhusu matumizi sahihi ya Kanuni 63 (3) na 63 (4) iliyotumiwa kuomba utaratibu.
Kishoa wakati wa mjadala katika madai yake dhidi ya Mwakyembe, alijenga hoja akirejea ripoti ya Mamlaka ya Usimamizi wa Manunuzi ya Umma (PPRA), ambayo alidai ililetwa kwenye kamati ambayo yeye ni mjumbe.
Aliendelea kudai kuwa licha ya mabehewa hayo kuwa feki, hata kampuni iliyopewa zabuni ya ununuzi huo haikukaguliwa. Kutokana na hasara hiyo, Kishoa alielekeza moja kwa moja kwa aliyekuwa Waziri wa Uchukuzi wakati huo Dk Mwakyembe akisema “taifa limeingia hasara ya bilioni 238 kwa sababu ya mtu tu kuwa mzembe kuwajibika, halafu leo jipu linahamishwa mkono wa kushoto linapelekwa mkono…” Aliendelea kusema,
“Magufuli atumbue majipu, na jipu limo humu ndani, tunaye Mheshimiwa Mwakyembe, lete ripoti hapa kuhusiana na masuala ya mabehewa. Mlikataa kuileta hapa kwa nini mnaficha... mheshimiwa Mwakyembe umeaminiwa na Serikali ya Magufuli, lete ripoti, haya mambo tunayakumbuka tuliona hata tukiwa nje”.