"Yapo
mengi ya kusema ila kwa leo nasema, pengo uliloliacha Mzee wetu Daniel Marwa Binagi tangu tarehe 06.02.2008
bado linaonekana na halitasahaulika kamwe. Mwenyezi Mungu Ailaze Roho yako
Pahala Pema Peponi, Amina! Ni mimi mwanao Mpendwa

George Marwa
Binagi (Pichani)".

Ilikuwa ni
Sekunde, Dakika, Masaa, Siku, Wiki, Mwaka hatimae hivi sasa ni miaka Minane imepita
tangu ututoke duniani Baba yetu Mpendwa, huku ukiacha kilio na majonzi kwa
wanao tuliokuwa bado wachanga ambao hakika ulituacha ilihali tukihitaji malezi
yako.

Ukiwa na
Miaka 83 mwaka 2008, Mzee wetu Mzee Daniel Marwa Binagi Mzaliwa na Mkazi wa
Kitongoji cha Chira Kata ya Turwa (Zamani), hivi sasa Kata ya Kenyamanyori
Wilaya ya Tarime Mkoani Mara Mwenyezi Mungu alikupenda zaidi na kukuchukua ili
ukapumzike baada ya kuteseka kwa maradhi katika kipindi cha muda mrefu.

Hakika
uliipenda na kuiongoza Familia yako bila ubaguzi wa aina yoyote. Ulionyesha
Mapenzi tele si tu kwa Wanao, Wajukuu zako, Wake zako bali kwa kila mmoja
aliekuzunguka ambapo uliweza kuonyesha mapenzi tele kwake huku tabia yako ya
kuchukia upuuzi na kuukumbatia ukweli ukikuongezea sifa rukuki kwa
waliokufahamu.

Ukiwa na
Elimu ya darasa la nne ambayo uliipata enzi za Mkoloni, uliweza kuleta
mapinduzi ya ajabu katika Kijiji chako na hata Wilaya ya Tarime na kuwa mmoja
wa Watu wenye Mafanikio makubwa Wilayani Tarime si tu kwa Kuwekeza katika
Ujenzi wa nyumba na Biashara katika mji wa Tarime bali hata katika Uungwana
wako.

Ulijizolea
sifa ya kuhakikisha kila mtoto anapata elimu kadri apendavyo na hivyo ndivyo
ilivyokuwa na ndiyo maana wakapatikana vijana mbalimbali kutoka katika uzao
wako wakiwa nafasi mbalimbali za utumishi ikiwa ni pamoja na wale walioingia
katika Sekta ya Elimu, Afya, Habari, Biashara, Urubani ikiwa ni miongoni mwa
taaluma mbalimbimbali huku wewe mwenyewe ukiamini katika mfumo wa Biashara, Kilimo
na Ufugaji.

Hakika wote
waliopata malezi yako wanajivunia mpaka leo kuwa na Mzazi kama wewe Mzee wetu
Daniel Marwa Binagi. Nakumbuka mambo mengi sana kutoka kwako ambayo ulikuwa
ukiwatendea wakati huo mimi nikiwa mdogo. 

Nilitamani sana kupata malezi yako
lakini Mwenyezi Mungu alikupenda zaidi. Nakumbuka namna ndugu zangu walivyosoma
katika Shule na Vyuo vizuri tena kwa gharama kubwa. Naogopa kusema sana ili
nisije nikakufuru ila nina kila sababu ya kusema kwamba pengine nami ningekuwa
mmoja wa wanao ambao wangesoma katika shule na vyuo vizuri kama ulivyokuwa
ukiniahidi wakati ukiwa kitandani unauguza maradhi yaliyokuwa yakikusibu.



Hakika Mzee
wetu wetu Daniel Marwa Binagi tututaendelea kukukumbuka kwa kuyaendeleza yale
yote mazuri uliyotuachia licha ya changamoto nyingi zinazojitokeza kutokana na
pengo lako. Yapo mengi ya kusema ila kwa leo nasema kwamba pengo uliloliacha
tangu tarehe 06.02.2008 bado linaonekana na halitasahaulika kamwe. Hakika
safari uliyoianza hapa duniani tangu tarehe 25.02.1925 ilifikia tamati mwaka
huo wa 2008. Mwenyezi Mungu Ailaze Roho yako Pahala Pema Peponi, Amina! 
Ni mimi
mwanao Mpendwa 
George Marwa Binagi.