Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa.
WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa ametangaza kuwa serikali imewalipa makandarasi Sh bilioni 400, ikiwa ni malimbikizo ya madeni yao. Amewaagiza makandarasi wote wa ujenzi wa barabara, waliokuwa wamesitisha kazi zao kutokana na madai yao, kurejea kazini mara moja.
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano imewalipa makandarasi hao Sh bilioni 400 kati ya deni lao la zaidi ya Sh trilioni moja ; na kwamba mpaka kufikia Juni mwaka huu, makandarasi wote watakuwa wamelipwa fedha zao.

Waziri Mbarawa aliyasema hayo juzi wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro, alipotembelea wilaya ya Mvomero kukagua uharibifu wa miundombinu ya barabara na daraja la Diwale lililopo eneo la Mvomero – Turiani.
Alisema kiasi cha fedha hizo zimelipwa kwa makandarasi mbalimbali nchini ili kuwawezesha wafanye kazi za ujenzi wa barabara zilizopo sehemu mbalimbali nchini. Profesa Mbarawa aliyefuatana na Naibu Waziri, Edwin Ngonyani alisema mradi wa ujenzi wa barabara ya Magole -Turiani ya kiwango cha lami yenye urefu wa kilometa 48.6 unaotekelezwa na mkandarasi, Kampuni ya Ujenzi ya M/S China Civil Engineering Construction Corporation Ltd (CCECC) ya China, tayari mkandarasi huyo amelipwa Dola za Marekani 735,243,357 na Sh 795,931,607.76 yakiwa ni malipo ya awali.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, malipo mengine yataendelea kutolewa baaada ya kupita wiki tatu ili kuwezesha kazi ya ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami kukamilishwa. Ujenzi wa barabara hiyo kwa kiwango cha lami, kwa sasa imejengwa urefu wa kilometa 13 pekee, wakati ujenzi huo ulitakiwa uwe tayari umekamilika na ulisimama kutokana na ukosefu wa fedha.
Waziri huyo pia alimuagiza mkandarasi anayesimamia ujenzi wa barabara hiyo, kumaliza kazi ya ujenzi wa daraja la Diwale ambalo liliharibiwa na mvua zinazoendelea kunyesha hivi karibuni na kukata mawasiliano baina ya pande mbili za tarafa ya Mvomero na Turiani.
Baadhi ya wananchi waliojenga kwenye hifadhi ya barabara kwa nyakati tofauti, walitoa kilio chao mbele ya waziri huyo, wakitaka kujua hatma yao kuhusu kubomolewa kwa nyumba zao. Akitoa kilio hicho kwa niaba ya wenzake, John Charles walimwomba Waziri kufikiriwa juu ya kulipwa fidia ili kuwaepushia usumbufu watakaoupata baaada ya kubomoa nyumba zao.
Akijibu malalamiko ya wananchi hao, Meneja wa Wakala wa Barabara (TANROADS) Mkoa wa Morogoro, Doroth Mtenga alisema sheria inaelekeza mtu yeyote haruhusiwi kufanya shughuli yoyote katika eneo la hifadhi ya barabara ndani ya mita 22 na nusu na kusisitiza kuwa Tanroads itawalipa wale tu waliofuatwa na ujenzi huo.