Lauren Bell

Mamia ya mashabiki wa kriketi nchini India wiki hii wamefurika kwenye mitandao ya kijamii kumsifu mkali wa England, Lauren Bell, wakimtaja kama mchezaji mrembo zaidi wa kriketi duniani baada ya kutangazwa kusaini mkataba na klabu ya Royal Challengers Bengaluru (RCB) kwa ajili ya msimu ujao wa Women’s Premier League (WPL).

Bell mwenye umri wa miaka 24 na urefu wa futi 6 na inchi 2, ni mchezaji wa kasi (seam bowler) na amenunuliwa kwa pauni 76,000 (Tsh480) katika mnada wa WPL uliofanyika Alhamisi.

Wachezaji wengine wa England waliopata dili ni pamoja na Sophie Ecclestone, aliyesajiliwa na UP Warriorz, Danni Wyatt-Hodge aliyejiunga na Gujarat Giants, na Nat Sciver-Brunt ambaye atasakata kriketi na mabingwa watetezi, Mumbai Indians.

Hata hivyo, ni usajili wa Bell ulioibua gumzo kubwa zaidi mtandaoni, baada ya mamia ya mashabiki nchini India kumiminika kwenye ukurasa wake wa Instagram kumpokea kwa shangwe.

“Mchezaji mrembo zaidi wa kriketi duniani sasa anachezea klabu nzuri zaidi, RCB,” aliandika shabiki mmoja.

“Tuna hamu kuona unavyotuwakilisha ndani ya timu ya RCB,” alisema mwingine.

Usajili wa Bell unatarajiwa kuipa RCB nguvu mpya na mvuto mkubwa kuelekea msimu ujao wa WPL.