Waziri wa Usalama wa Ndani wa Marekani, Kristi Noem, ametangaza kuwa amependekeza kwa Rais Donald Trump kuweka marufuku ya usafiri bila ubaguzi dhidi ya mataifa anayodai yanaiingizia Marekani wahalifu na watu wasiokuwa na mchango kwa taifa hilo.

Noem hakubainisha ni nchi gani zitakazojumuishwa, lakini kauli hiyo imekuja kufuatia tukio la kushambuliwa kwa askari wawili wa Jeshi la Akiba (National Guard) mjini Washington DC wiki iliyopita.

Kupitia taarifa aliyochapisha kwenye mitandao ya kijamii mara baada ya kukutana na Trump, Noem alisema:
“Nimemaliza mazungumzo na Rais. Ninashauri marufuku kamili ya usafiri dhidi ya kila nchi inayotuma wahalifu, watu wasiokuwa na tija, na wanaotegemea misaada bila kutoa mchango wowote.”

Waziri wa Usalama wa Ndani wa Marekani, Kristi Noem.

Hatua hiyo imeibuka siku chache baada ya Rais Trump kutangaza kusimamisha kwa muda uhamiaji wote kutoka Afghanistan, pamoja na maombi ya hadhi ya ukimbizi, kufuatia shambulio lililotokea wiki iliyopita katika jiji la Washington.

Aidha, Trump ameahidi “kusitisha kabisa uhamiaji” kutoka nchi maskini za dunia, huku akieleza kuwa maombi ya wahamiaji kutoka mataifa 19 yaliyowahi kuwa kwenye orodha ya marufuku ya usafiri wakati wa utawala wake wa awali sasa yatapitiwa upya.

Mataifa hayo ni pamoja na Afghanistan, Iran, Somalia, Haiti, Sudan, Yemen, Libya na Venezuela, pamoja na mengine kadhaa.