Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky amemshukuru Waziri Mkuu wa Ireland Micheál Martin kwa makaribisho, na kusema ziara yake inafanyika kama moja "yenye changamoto" na bado " ina matumaini".

"Sasa kuliko wakati mwingine wowote, kuna fursa ya kumaliza vita hivi," alisema.

Kwenye mpango wa amani, anasema baadhi ya mambo "bado yanahitaji kutatuliwa", lakini anasema Marekani inachukua hatua za dhati kumaliza vita "kwa njia moja au nyingine".

Aliongeza kuwa Ukraine ina matamanio ya kuwa mwanachama wa EU ndani ya miaka mitano ijayo.

Kwa upande wake, Micheál Martin alishutumu "kutojali kabisa" kwa Putin kwa sheria za kimataifa, na kusema kwamba rais wa Urusi "kamwe asiruhusiwe kufanikisha" matakwa yake.

Aliongeza kuwa leo atatia saini mkataba wa ushirikiano na Ukraine, akiongeza msaada wa kifedha kwa nchi hiyo kwa €125m (£110m)

Kuhusu mazungumzo ya Marekani na Urusi yaliyofanyika leo, Zelensky alisema anatarajia Marekani kuripoti kwake baada ya mkutano huo - na hatua za baadaye za kufikia amani zinategemea hili.