Wizara ya Viwanda na Biashara, inatarajia kufanya operesheni maalum ya kuziondoa na kuziteketeza bidhaa zote zinazoingizwa nchini zisizokuwa na ubora na viwango.
Hatua hiyo itachukuliwa kwa lengo la kumlinda mtumiaji kutokana na madhara yanayoweza kutokea.
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam na Waziri wa Viwanda na Biashara Dk. Cyril Chami, alipotembelea Shirika la Viwango Tanzania (TBS) mwishoni mwa wiki.
Dk. Chami alisema kumekuwapo na idadi kubwa ya bidhaa feki na zisizokuwa na viwango jambo ambalo ni hatari kwa za watumiaji.
Alisema umefika wakati wa kuziondoa bidhaa zote zisizokidhi viwango vya ubora.
"Serikali imejipanga kuziondoa na kuziteketeza bidhaa zote zisizokuwa na viwango vinavyotakiwa na hii itawasaidia wafanyabiashara kuhakikisha kuwa bidhaa wanazoingiza nchini zinakuwa na ubora," alisema.
Dk. Chami alisema TBS inatakiwa kufanya kazi kwa ukaribu na Mamlaka ya Mapato nchini (TRA) kuhakikisha bidhaa zote zinazoingia nchini zinakuwa na ubora unaotakiwa.
Alisema ongezeko la bidhaa feki nchini linatokana na rushwa ambapo mfanyabiashara anapokatwa hutoa fedha na bidhaa zake kuachiwa na hivyo kuendela kuzagaa madukani.
Alisema Wizara yake pamoja na Wizara ya Kilimo na Chakula, Mamlaka ya Chakula na dawa (TFDA), TRA na TBS, watashirikiana ili kuhakikisha kunakuwa na bidhaa zenye ubora.
Dk. Chami alisema atatoa mapendekezo kwa Rais wa Zanzibar ili TBS ifanye kazi zake visiwani kwa kukagua na kudhibiti bidhaa zote zisizokuwa na viwango kutoingia Zanzibar.
0 Comments